Trump: Tuko nyuma lakini hatukati tamaa

Trump supporters in Cleveland

Maafisa wa kampeni wa mgombea urais wa chama cha Republican nchini Donald Trump wamekiri kwamba mgombea huyo yupo nyuma ya mpinzani wake Hillary Clinton wa chama cha Democratic zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi kufanyika.

"Tuko nyuma. Kuna baadhi ya mambo ambayo yanamfaa yeye (Bi Clinton)," meneja wa kampeni wa Bw Trump, Kellyanne Conway amesema.

Hata hivyo, ameongeza: "Hatukati tamaa. Tunajua kwamba tunaweza kushinda."

Mnamo Ijumaa, Bw Trump alionekana kukiri uwezekano kwamba anaweza kushindwa.

Alisema iwapo atashinda, ashindwe au atoshane nguvu na mpinzani wake, ataridhishwa na juhudi zake.

Siku moja baadaye, alitangaza hatua ambazo atazichukua siku 100 akiwa uongozini iwapo atashinda.

Miongoni mwa hizo ni kuweka masharti mapya kwenye mchakato wa kisiasa wa kutafuta uungwaji mkono kisiasa, mikataba ya kibiashara na mabadiliko ya tabia nchi.

Kura mpya za maoni zinaonesha Bi Clinton yupo mbele sana kitaifa na katika majimbo mengi yanayoshindaniwa.

Maafisa wake kampeni wa Clinton wamebashiri kwamba huu utakuwa "uchaguzi mkubwa zaidi katika historia ya Marekani".

Meneja wake wa kampeni Robbie Mook aliambia Fox News Jumapili: "Watu watajitokeza kupiga kura zaidi ya wakati wowote awali."

Kura za maoni katika majimbo ambayo ni ngome ya chama cha Republican kwa mfano Utah na Arizona zinaonyesha huenda majimbo kwa mara ya kwanza katika miongo mingi akaunga mkono mgombea wa Democratic.

Arizona kubadilika

Kura za maoni Arizona zinaweza zikawa si sahihi lakini iwapo ni sahihi, basi jimbo hilo huenda likaanzisha mtindo wa kura utakaomfaa Clinton mwaka 2016 na hapo baadaye kuwa jimbo la kushindaniwa.

Sana, hilo linatokana na kuongezeka wa wapiga kura wa asili ya Kilatino (Hispania).

Kwa chama cha Democratic, hizo zitakuwa habari njema sana na ambazo zitasaidia katika uchaguzi.

Lakini kwa Republican, huenda ukawa mwanzo wa masaibu ya kisiasa.

Zikiwa zimesalia siku 16 pekee kabla ya uchaguzi, macho ya wengi yanaelekezwa sana kwenye kashfa ambazo zimehusishwa na kampeni za Bw Trump.

Jumamosi, aliapa kwamba atawashtaki wanawake waliomtuhumu kuwa aliwadhalilisha kingono.

Aidha, alirejelea madai yake ya awali kwamba uchaguzi umeibwa na kwamba ulaghai wa kura unafanyika vituoni na kupitia vyombo vya habari kwenye mapendeleo.

Jumapili, mwanawe Eric Trump alisema babake atakubali matokeo ikiwa tu uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Nini kinafuata?

  • Wagombea wanatarajiwa kutumia siku 16 zilizosalia kujipigia debe. Wanatarajiwa kupiga kampeni sana majimbo yanayoshindaniwa kama vile Ohio, Carolina Kaskazini, Florida na Pennsylvania
  • Uchaguzi utafanyika Jumanne 8 Novemba kuamua Rais wa 45 wa Marekani.
  • Rais mpya ataapishwa 20 Januari 2017