Maafisa: Al-Shabaab sio waliotekeleza shambulio la Mandera

Washambuliaji walirusha vilipuzi kwenye jumba hilo Haki miliki ya picha Ibrahim Adan Ali / Key FM
Image caption Washambuliaji walirusha vilipuzi kwenye jumba hilo

Shambulio la usiku katika mji wa Mandera nchini Kenya limetekelezwa na wanamgambo wasio al-Shabab, kwa mujibu wa mratibu wa usalama wa eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya Bw Mohamud Saleh.

Mandera inapakana na Ethiopia na Somalia.

Kundi la Al-Shabab Somalia tayari limekiri kuhusikana shambulio hilo dhidi ya nyumba ya malazi , kama tulivyoarifu awali.

Lakini Bwana Saleh amesema kutokana kuwa mpka na Somalia hufungwa kuanzia usiku hadi alfajiri , hakuna namna kwa washambuliaji kuvuka mpaka huo.

Ameongeza kuwa uchunguz wa awali umedhihirisha kuwa shambulio hilo la saa tisa alfajiri lilitekelezwa na "magengi ya wahalifu walio na itikadi kali waliopo katika mji wa Mandera ambao wametumia vilipuzi vinne kuilipia nyumba hiyo ya malazi".

Watu 12 wameuawa baada ya watu wenye silaha kushambulia nyumba hiyo ya malazi mjini Mandera.

Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe amesema watu sita wameokolewa kutoka kwenye hoteli hiyo ya Bishaaro.

Wanamgambo walirusha vilipuzi kwenye nyumba hiyo kabla ya kuingia ndani na kuanza kuwafyatulia risasi waliokuwemo ndani.

"Sehemu ya jumba iliporomoka, na kuua watu 12. Watu sita wametolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo hilo wakiwa hai kufikia sasa," ameandika Bw Kiraithe kupitia mtandao wa Twitter.

Wataalamu wa mabomu wanafanya uchunguzi kubaini ni vilipuzi vya aina gani vilitumiwa kutekeleza shambulio hilo.

Image caption Mji wa Mandera unapatikana katika mpaka wa Kenya, Somalia na Ethiopia

Awali kundi la al-Shabaab limekiri kutekeleza shambulio hilo.

Mji wa Mandera umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na wanamgambo wa al-Shabaab, kundi linalopigana dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika taifa jirani la Somalia.

Wanamgambo hao wamekuwa wakishambulia watu ambao si wa asili ya Kisomali.

Haki miliki ya picha Ibrahim Adan Ali / Key FM
Image caption Maafisa wa usalama nje ya hoteli ya Bishaaro

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii