Watu kadhaa wauawa katika shambulio la wanamgambo Quetta

Wamefikishwa katika hospitali iliyo karibu na eneo hilo Haki miliki ya picha EPA
Image caption Wamefikishwa katika hospitali iliyo karibu na eneo hilo

Takriban makada 58 katika jeshi na walinzi wameuawa baada ya wanamgambo kukishambulia chuo cha polisi katika mji wa Quetta, Pakistan, maafisa wanasema

Wanamgambo watatu waliojihami kwa mabomu waliingia ndani ya chuo hicho Jumatatu na kuarifiwa kuwachukua watu kadhaa mateka.

Washambuliaji hao waliuawa katika operesheni kubwa ya usalama iliochukua saa kadhaa.

Hakuna kundi lililokiri kutekeleza shambulio hilo, lakini kumeshuhudiwa mashambulio kama hayo katika mji wa Quetta yaliotekelezwa na wanamgambo wanaotaka kujitenga na wenye itikadi kali za dini ya kiislamu katika miaka ya hivi karibuni.

Mamia ya wanafunzi walihamishwa kutoka chuo cha polisi cha Balochistan wakati wanajeshiw walipowasili kupambana na wanamgambo hao.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa

Vyombo vya habari katika eneo hilo vinaripoti kuwa kumetokea miipuko takruban mitatu katika eneo la mkasa.

"Niliona wanaume watatu waliovaa nguo za kijeshi na wakiwa wamebeba bunduki aina ya Kalashnikovs," Kada mmoja alisema kwa mujibu wa shirka la habari la AFP. " Walianza kufyetua risasi na kuingia katika bweni lakini nilifanikiwa kutoroka kwa kuruka ukuta."

Kuna mamia ya wanafunzi katika chuo hicho na makada wengi waliofariki waliuawa katika mlipuko, amesema Meja jenerali Sher Afgan.

Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES
Image caption Operesheni ya polisi ilichukua saa kadhaa
Haki miliki ya picha AFP/GETTY IMAGES

Haijulikani jinsi hali ilivyojiri lakini ni wazi kuwa kulikuwa na ufyetuaji wa risasi kati ya washambuliaji na vikosi vya usalama kwa saa kadhaa kwa mujibu wa gazeti la Dawn.

Pia kuna taarifa kuwa kuna watu wamezuiwa mateka.

Zaidi ya watu 100, wengi wao wanafunzi wamejeruhiwa.

Wanamgambo wawili walifariki baada ya kulipua mabomu waliovaa na mmoja aliuawa na vikosi vya usalama.