Raia wa Rwanda aliyefungwa miaka 25 Ufaransa akata rufaa

Pascal Simbikangwa Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pascal Simbikangwa alikuwa mkuu wa idara ya upelelezi Rwanda

Mahakama nchini Ufaransa imeanza kusikiliza kesi ya rufaa iliyowasilishwa na Pascal Simbikangwa raia wa Rwanda akipinga hukumu ya kifungo cha miaka 25 jela aliyopewa na mahakama mjini Paris miaka 2 iliyopita kwa kupatikana na hatia ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.

Kesi hiyo dhidi ya Simbikangwa ilikuwa ya kwanza katika historia ya Ufaransa ikihusu mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari.

Katika kesi ya awali mahakama ilimpata na hatia ya kushirikiana na watu wa kabila la Wahutu wenye msimamo mkali waliopanga na kutekeleza mauaji ya kimbari.

Pia alipatikana na hatia ya kugawa silaha kwa makundi ya wanamgambo wa Interahamwe na kutoa amri kwenye vizuizi vya barabarani kwa ajili ya kuzuia waliokuwa wanakimbia mauaji hayo.

Hoja za upande wa utetezi zilikuwa kwamba mshukiwa hakuhusika kamwe katika mauaji ya kimbari na yeye husisitiza kwamba hakuona maiti hata moja mjini Kigali.

Mashirika ya kutetea haki za manusura wa mauaji ya kimbari nchini Ufaransa na mawakili wao wanadai hakuna budi mahakama kuongeza hukumu hiyo hadi kifungo cha maisha.

Simbikangwa mwenye umri wa miaka 54 alikuwa afisa katika jeshi la ulinzi la rais wa zamani wa Rwanda Juvenal Habyarimana akiwa na cheo cha kapteni na alihudumu pia kama mkuu wa idara ya upelelezi.

Mwezi wa saba mwaka huu mahakama ya Ufaransa pia iliwapa kifungo cha maisha jela raia wengine 2 wa Rwanda Octavien Ngenzi na Tito Barahira kwa kuwakuta na hatia ya mauaji ya kimbari.