Natasha Annie Tonthola: Vita vyangu dhidi ya 'fisi mtu' Malawi

Bi Natasha Annie Tonthola, akielimisha umma nchini Malawi Haki miliki ya picha ELDSON CHAGARA
Image caption Bi Natasha Annie Tonthola, akielimisha umma nchini Malawi

Mwezi Julai BBC iliripoti kuhusu mwanamume mmoja raia wa Malawi anayelipwa ili kufanya ngono na wasichana kutoka katika kijiji chake, kama sehemu ya tambiko la wasichana kubaleghe.

Baadaye mwanamke mmoja wa Malawi, Natasha Annie Tonthola, aliwasiliana na BBC kuelezea namna alivyopitia uchungu katika matambiko hayo, na jinsi ulivyomsaidia kuanzisha kampeini ya kuwalinda wanawake na wasichana.

Hi hapa hadithi yake.

Mimi ni mzaliwa wa kwanza kati ya watoto watano, na nilikulia kijijini maeneo ya kati kati nchini Malawi karibu na mji mkuu Lilongwe.

Nilikuwa na umri wa miaka 13 nilipofanyiwa sherehe ya tambiko la kubaleghe.

Babangu alitokea kijiji kilichoko karibu na Mulanje, kusini mwa nchi, na nilitumwa huko kwa sherehe hiyo, mara tu baada ya kupata hedhi kwa mara ya kwanza. Huna uamuzi - Wasichana wote wa kijijini wamekabiliwa na tambiko hiyo.

Haki miliki ya picha Empics
Image caption Ramani ndogo ya malawi

Tuliambiwa kuwa tunakwenda kujifunza namna ya kuwa mwanamke, na kwa kweli nilifurahi sana. Na hali huwa hivyo kwa kila msichana.

Siku ya mwisho, mmoja wa wanawake wazee alituambia kuwa tumefika mwisho wa mafunzo.

Alisema kuwa Fisi atakuja kututembelea. "Msiogope, sizungumzii juu ya mnyama," alisema. "Namaanisha mwanamume."

Lakini hatukujua kwa hakika fisi ni nini, au anakuja kufanya nini.

Huelezwi kuwa anakuja kufanya ngono na wewe.

Mama huyo mzee anaingia ndani na kusema, 'Hongera, mmemaliza sherehe ya kufuzu, sasa mmekuwa wanawake'.

Kila mmoja tulikuwa na kitambaa na tukaambiwa tulaze chini sakafuni. Tukaambiwa sasa muda umewadia wa kuonyesha namna ya kumhudumia mwanamume.

Tulivyo fahamishwa namna ya kuwafanyia waume wetu siku za usoni.

Hapo tukazibwa nyuso zetu.

Hatukufaa kuonyesha kwamba tumeshtuka, haufai pia kuonyesha kuwa haujui utakacho fanyiwa.

Kisha mwanamume anakuja, na anakuambia ulale chini, unapanua miguu na anaanza kufanya anachofanya. Hatupaswi kujua mwanamume huyo ni nani- ni wazee tu ndio wanaomfahamu.

Tulikuwa wasichana wadogo, kwa hivyo tulikuwa na uwoga mwingi, na mtu huyo alifungua miguu yetu kwa nguvu. Nilihisi uchungu mwingi sana. Alipomaliza, nilisikia nafuu. Mama huyo mzee alikuja na kusema,"hongera mmemaliza vyema sherehe hii ya kufuzu na sasa mmekuwa wanawake."

Wasichana wengi wanadhani ni kawaida, tukidhani ni kudumisha utamaduni wetu lakini tumepotoshwa.

Fisi hakutumia mpira, na baadhi ya wasichana walishika mimba.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kina mama wa umri mdogo

Tulipofika nyumbani, hatukuruhusiwa kuzungumza wala kucheza na wasichana ambao hawajakwenda au kupitia tambiko hilo. Sikuruhusiwa kumwambia dadangu mdogo jambo lolote kuhusiana na hilo.

Wasichana wanaanza kuvunja ungo mapema, wanapata hedhi wakiwa bado wadogo, sasa wasichana wa hata umri wa miaka 10 au 11 hupitia tambiko hili.

Baada ya sherehe hiyo, maisha yangu yalichukua mkondo m'baya sana. Babangu aliyekuwa afisa wa polisi, alifariki mwaka uliofuatia.

Tabia ya "kurithi wanawake" inasema kuwa, kakake mtu anayefariki, anafaa kumuoa mjane aliyeachwa, ili kusaidia familia, lakini mamangu alikataa katu kufuata tamaduni hiyo.

Badala yake tulihamia Afrika Kusini, kwani mamangu alikuwa nusu Muafrika Kusini na mjombangu alituita huko kuanza maisha upya.

Tulianza kufanya kazi ili kujikimu kimaisha- nilidanganya kuhusu umri wangu na nikapata kazi kwenye chumba cha ususi na jikoni. Pia nilifanya kazi kama mjakazi wa nyumbani.

Lakini licha ya kufanya kazi kwa bidii, hatukupata pesa za kutosha kulipa karo au kuisaidia familia.

Kisha, kupitia jamaa zetu nchini Malawi, nilibaini kuwa kulikuwa na mwanamume aliyekuwa radhi kunilipia karo kwa makubaliano kuwa atanioa baadaye.

Nilikuwa ninakaribia umri wa miaka 16 , na sikutaka kuolewa katika umri huo mdogo, wala mamangu pia hakutaka.

Lakini nilikuwa natamani sana kukamilisha masomo yangu, nilikuwa na wasiwasi kuhusu ndugu zangu pamoja na mama yangu, ambaye alifanya kazi kwa bidii mno, na akaanza kutatizika kiafya.

Kwa hivyo nilikubali na sote tukarejea tena Malawi.

Katika baadhi ya jamii walituambia: 'usidhani kuwa, kwa sababu umeelimika, utatuambia kitu cha kufanya'

Ndoa ya utotoni

Tulifanya ndoa ya kitamaduni na akaanza kunilipia karo ya shule ya upili na kusaidia familia yangu. Alikuwa miaka 15 zaidi yangu na mtu aliye elimika, mfanyabiashara maarufu, lakini alikuwa akinichapa mara kwa mara.

Bado ningali na alama nyingi mwilini kutokana na ndoa hiyo.

Nilipata mimba nilipokuwa na umri wa miaka 17. Mume wangu alikuwa bado akinipiga- nusura mimba itoke - na alikuwa akifanya ngono muda wote nilipokuwa mja mzito- lakini uzuri ni kwamba, nilifaulu kufanya mtihani wangu wa mwisho kabla ya kumzaa binti yangu.

Nilikata tamaa. Sikutaka maisha yangu yawe hivyo, na nilifahamu fika kuwa mume wangu alitekeleza hayo yote, kwa sababu nilikuwa bado mchanga na katika hatari ya dhuluma kama hiyo, huku nikiwa sina mahali pengine pa kwenda.

Nilikuwa nimenaswa katika mtego.

Hapo ndipo mjomba wangu wa Afrika Kusini, alipofika na kuniokoa tena.

Alielewa kuwa nilitamani sana kuwa mwanamitindo, na akanisaidia kujiunga na chuo cha mafunzo ya mitindo ya nguo.

Siku zote mume wangu alinitishia kuwa nikimwaacha, atanisaka na kuniuwa. Kwa hivyo niliamua kumdanganya, "nitakuja nyumbani katika kipindi cha wiki moja au mbili hivi.

Lakini sikwenda, badala yake nilisomea taaluma hiyo, na nikapata kazi katika mgahawa mmoja.

Baadaye nikarudi Malawi na nikaanzisha biashara ya kushona nguo, huku nikiwa na wateja matajiri na wenye sifa na hadhi.

Pia nikafungua mgahawa- ninapenda sana upishi na ni njia mojawepo ya kukabiliana na msongo wa mawazo.

Nikaanzisha shirika la kijamii , linaloshughulikia matatizo kadha wa kadha, kama vile kuwafanya watoto wasichana kusalia mashuleni, kwa kukabiliana na ndoa za mapema, kuelimisha jamii kuhusiana na tamaduni pamoja na matambiko yaliyopitwa na wakati - kama ya fisi- inayohatarisha maisha ya wasichana, na uhamasisho dhidi ya virusi vya HIV na ukimwi, mimba za mapema na afya ya uzazi.

Msuko suko na mume wangu ulikuwa ungalipo. Mara tu alipogundua kuwa nimerejea Malawi, alianza kuniandama. Alisema maneno kama: "ikiwa sitaishi nawe, hakuna mwengine yule atakayeishi nawe."

Siku moja alifika nyumbani kwangu nilikoishi, sijui alipataje kujua, lakini alionekana mtulivu, kwa hivyo nikamruhusu akaingia ndani. Alisema alitaka kuniona, na pia kumuona binti yangu, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka mitatu. Alisema kuwa ananipenda, huku akiniomba msamaha na kukiri kuwa ni mtu aliyebadilika.

"Bado tungali tumeoana, na nimekufanyia mengi," alisema. "Kama sio mimi, niliyekulipia karo na kusaidia familia yako, haungekuwa hivi ulivyo leo. Ninakudai."

Nilimuambia: "baada ya mateso hayo yote, sasa nakuogopa sana."

Kwa hakika, sikutaka kurejea kwake ili kuishi naye tena. Alifyoka, akatupa vitu kiholela na akaanza kunikaba koo- licha ya kuwa, nilikuwa nimempakata binti yangu. Angeniuwa ikiwa majirani hawangeitikia kamsa. Waliingia kwa nguvu nyumbani na kumtupa nje. Sikumshtaki, kwani sikutaka kuweka kesi yangu waziwazi hata ingawa ilikuwa tayari inajulikana.

Lakini nilipata ilani ya kumzuia kutofika kwangu.

Muda huu wote, nilihisi msukumo ndani yangu kuwa yote haya yanayofanyika maishani mwangu, kunao wasichana na wanawake ambao pia wanapitia masaibu kama hayo.

Changamoto

Shirika langu liliendelea kuwaelimisha watu, japo kwa ugumu sana, hasa tunapokinzana na tamaduni kama vile matumizi yaafisi na tabia ya kuwarithi wanawake wajane.

Tulisambaza visodo vingi sana.

Katika baadhi ya jamii walituambia: 'usidhani kuwa, kwa sababu umeelimika, utatuambia kitu cha kufanya'

Mila na desturi hii, imekuwepo kwa miaka na mikaka, na tumetekeleza kwa muda mrefu bila ya matatizo."

Haki miliki ya picha ELDISON CHAGARA
Image caption Natasha Annie Tonthola

Lakini baadhi ya wazee na madhehebu kadhaa, yalikomesha tamaduni hizo katika vijiji vyao.

Katika kazi yangu ya kuhudumia jamii, nilifahamu kuwa vizingiti vingi vinawakumba watoto wa kike walioko shule. Ikiwa familia inapitia changamoto ya kifedha, kuna uwezekano mkubwa kuwa, watawalipia karo watoto wavulana badala ya wasichana.

Ikiwa msichana anaacha shule, pana uwezekano mkubwa kwa familia kumuoza, badala ya kumuona akiwa nyumbani siku nzima. Na wasichana wengi wanakosa kwenda darasani kwa sababu ya hedhi, kwani hawawezi kununua visodo.

Ili kujaribu kutanzua tatizo hili, mojawepo ya vitu vikuu, ambavyo shirika langu linashughulikia ni kusambaza visodo na nguo za ndani, ambazo zinaweza kuoshwa ili zitumike tena na hazichafui mazingira.

Mwaka 2011, nilifahamu kuwa ninafaa kuanzisha shirika rasmi na hapo ndio ikawa mwanzo wa wakfu wa Mama Africa. Ninauita ubunifu huu kama mradi wa heshima.

Licha ya yote yaliyofanyika, nina matumaini kuwa hali itakuwa nzuri siku zijazo.

Nadhani kuna mengi ambayo tunaweza kufanya kwa ajili ya wanawake na watoto ambao ni waathiriwa wa fisi, dhuluma za kijinsia, na maovu mengine mengi katika jamii, pamoja na changamoto chungu nzima.

Ni hatua ngumu mno, lakini ningali na matumaini.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii