Mchina atozwa faini kwa kuuza bendera za Zimbabwe

Bendera ya Zimbabwe Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bendera ya Zimbabwe

Raia mmoja wa Uchina amekuwa mtu wa kwanza kutozwa faini kwa kuuza bendera za Zimbabwe bila rukhusa rasmi kulingana na gazeti la taifa la Herald.

Mfanyibiashara huyo alipigwa faini ya dola 20 huku takriban bendera 314 zikinaswa,ilisema.

Mwezi uliopita serikali ya Zimbabwe ilionya kwamba mtu yeyote atakayeagiza nje,kutengeza ama hata kuuza bendera ya taifa hilo bila rukhusa ama kuichoma mbali na kuiharibu atashtakiwa.

Onyo hilo linajiri baada ya kundi moja kufanya maandamano likitumia bendera hizo likitaka uongozi wa rais Mugabe wa miaka 36 kusitishwa.

Vuguvugu hilo lilianza katika mitandao ya kijamii likitumia hashtag #ThisFlag na kutoa wito kwa raia wa Zimbabwe kumiliki bendera zao ili kuwashinikiza wanasiasa kujibu maswali kuhusu kutowajibika kwao na ufisadi bila hofu.