Mauzo ya Coca Cola yaendelea kushuka

Coca-Cola Haki miliki ya picha Getty Images

Mauzo ya vinywaji vya kampuni ya Coca-Cola yameshuka kwa 7% na kufikia $10.6bn katika kipindi cha miezi mitatu kufikia mwezi Septemba, huku wateja wakionekana kupunguza unywaji wa soda na vinywaji vingine vyenye kaboni.

Hii ni robo ya sita mfululizo kwa mapato ya kampuni hiyo kushuka.

Mauzo yalishuka Amerika Kusini, Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika kwa takriban asilimia nne, ingawa mauzo Marekani Kaskazini yaliongezeka kwa asilimia tatu na barani Asia yakaongezeka kwa asilimia nne.

Maji na vinywaji vya kutumiwa michezoni vilichangia ongezeko la asilimia tatu katika mauzo ya vinywaji visivyo na kaboni.

Faida baada ya kutozwa ushuru ilishuka 28% hadi $1.05bn (£859m) katika robo hiyo iliyomalizika Septemba.

Hata hivyo, mapato pamoja na faida yalikuwa heri kuliko walivyokuwa wamekadiria wadadisi, na hilo lilichangia kupanda kwa bei ya hisa za kampuni hiyo soko la hisa la New York kwa asilimia moja hadi $42.88.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mauzo ya vinywaji vyenye kaboni kama vile Sprite, Fanta na Coca-Cola Zero ndiyo yaliyochangia ongezeko la mauzo la asilimia tatu Amerika Kaskazini na kufikia $2.66bn, lakini mauzo ya Diet Coke yalishuka.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii