Msimamizi wa jumba lililovamiwa Mandera, Kenya akamatwa

Jamaa na marafiki wa waliouawa walifika kutambua miili Chiromo, Nairobi mnamo Jumatano
Image caption Jamaa na marafiki wa waliouawa walifika kutambua miili Chiromo, Nairobi mnamo Jumatano

Msimamizi wa nyumba ya malazi iliyoshambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la al-Shabaab mjini Mandera, ambapo watu 12 waliuawa, amekamatwa.

Bw Abdirahman Bishar Ali, ambaye amekuwa msimamizi wa gesti ya Bisharo amekamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kusaidia katika utekelezaji wa shambulio hilo.

Stakabadhi ya polisi zinasema Bw Ali hakulala kwenye gesti hiyo kama ilivyo kawaida yake usiku wa shambulio.

"Alilala kwenye nyumba jirani iliyo umbali wa mita 15 kutoka gesti ya Bisharoo na hakufanya hatua zozote kupiga ripoti kwa polisi," stakabadhi za waendesha mashtaka zinasema.

Washambuliaji waliwalenga watu wa kutoka nje ya mji huo wasio wa asili ya Kisomali.

Image caption Maafisa wa usalama wakiwa nje gesti ya Bishaaro baada ya shambulio

Kundi la al-Shabaab ambalo limekuwa likipiga vita serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Somalia limedai kuhusika.

Mkuu wa jimbo la kaskazini mashariki Mohammud Saleh hata hivyo alifutilia mbali uwezekano wa wapiganaji hao kutoka Somalia kuwa ndio waliotekeleza shambulio hilo.

Badala yake, alisema lilitekelezwa na "magenge ya wenyeji".