Benki ya Dunia: Kenya imerahisisha sana biashara

Mohammed
Image caption Mohammed, 28, mwuzaji wa vipuri vya simu jijini Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua kuhusu mikopo

Benki ya Dunia imeitaja Kenya kama moja ya nchi zilizochukua hatua madhubuti kurahisisha uendeshaji wa biashara. Tanzania pia imesifiwa kwa mageuzi kuhusu mikopo.

Benki hiyo kwenye ripoti yake ya urahisi wa kuendesha biashara ya mwaka 2017 inasema Kenya ni miongoni mwa nchi kumi zilizoboresha zaidi mifumo yake ya sheria za kusimamia uendeshaji biashara.

Nchi hizo nyingine ni Brunei Darussalam, Kazakhstan, Belarus, Indonesia, Serbia, Georgia, Pakistan, Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE) na Bahrain.

Kenya kwa sasa imeorodheshwa nambari 92 kwenye orodha hiyo inayoongozwa na New Zealand ikifuatwa na Singapore.

Mwaka uliopita, Kenya ilikuwa imeorodheshwa nambari 108.

Tanzania imepanda kutoka nambari 139 mwaka uliopita hadi mwaka 132.

Rwnada imo nambari 56, Afrika Kusini 74, Ghana 108, Uganda 115, Malawi 133, Msumbiji 137, Burundi 157 na Ethiopia 159. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imo nambari 184.

Miongoni mwa mengine, Kenya imesifiwa kwa kupunguza masharti ya kuanzisha biashara.

"Kwa kufanyia marekebisho sheria iliyohitaji stakabadhi za kufungua biashara zitiwe saini na afisa wa kiapo, Ireland, kenya na Uganda zilipunguza pakubwa muda unaohitajika na wajasiriamali kufungua biashara," ripoti hiyo inasema.

Image caption Mafundi wa magari jijini Nairobi. Kenya imerahisisha sana utaratibu wa kuanzisha biashara

Hata hivyo, kwa kiasi fulani, iliifanya vigumu kuanzisha biashara kwa kuweka ada ya jumla ya kurasmisha kampuni.

Kenya pia imerahisisha shughuli ya kupata umeme, kusajili mali na pia kuweka mikakati ya kuwalinda wawekezaji wadogo.

Tanzania imepiga hatua zaidi katika kupanua fursa za watu kukopa pesa.

Wakala wa habari kuhusu mikopo Tanzania Creditinfo, alipanua maelezo kuhusu mikopo kutoka kwa 4.97% ya raia wote hadi 6.48%. Hili sana lilifanikishwa na kutiwa saini kwa mikataba kati ya wauzaji wa rejareja na wafanyabiashara wengine kutoa maelezo ya wateja kuhusu mikopo.

Hata hivyo, Tanzania imekosolewa kwa kuifanya vigumu kwa watu kulipa kodi.