Mkewe rais wa zamani wa Nigeria ashtaki kuzuiwa mali yake

Patience Jonathan Haki miliki ya picha AFP

Mke wa aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan - Patience Jonathan analishtakia shirika la kupambana na rushwa nchini kima cha dola milioni 200 kwa kuzuia fedha katika baadhi ya akaunti zake za benki , gazeti la kibinafsi la Vanguard linaripoti.

Amewasilisha nyaraka mahakamani , akitaka tume hiyo ya kupambana na rushwa Nigeria, (EFCC) kumruhusu kutumia fedha zake na zimlipe fedha kwa kukiuka haki zake.

Takriban wanawake 100 waliandamana nje ya mahakama kuu katika mji mkuu Lagos, kuonyesha kusimama kwao na Bi Jonathan.

Tume ya EFCC ilizuia baadhi ya akaunti zake mnamo Septemba 22 ilipokuwa ikichunguza tuhuma dhidi yake za kuendesha biashara haramu ya pesa.

Taarifa wakati huo zilikuwa ni kwamba dola zake milioni 15 zilizuiwa.

Amekana kutenda makosa yoyote.

Jaji ametaja Desemba 7 kama tarehe ya kusikizwa kesi yake dhidi ya tume ya EFCC.

Mwaka jana, mumewe Goodluck Jonathan alikuwa rais wa kwanza madarakani Nigeria kusalimu kwa hiari uongozi baada ya kushindwa katika uchaguzi.

Kiongozi aliyemrithi Muhammadu Buhari alishinda katika uchaguzi huo kwa ahadi yake kuwa atapambana na rushwa.