Wanawake wa Yazidi wameshinda tuzo ya Sakharov

Nadia Murad Bansee Taha mshidni wa tuzo ya Sakharov. Haki miliki ya picha EPA

Wanawake wawili wa kabila la Yazidi waliotoroka utumwa wa kingono uliotekelezwa na kundi la Islamic State (IS) nchini Iraq wameshinda tuzo kuu ya Ulaya ya haki za Binaadamu, tuzo ya Sakharov.

Nadia Murad Basee na Lamiya Aji Bashar wlikuwa miongoni mwa maelfu ya wasichana na wanawake wa kabila la Yazidi waliotekwa na wanamgambo wa IS na kulazimishwa kuingia katika utumwa wa kingono mnamo 2014.

Lakini wote walifanikiwa kutoroka na sasa wanaifanyia jamii ya Yazidi kampeni.

Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka katika kumkumbuka Andrei Sakharov, mwasayansi wa iliyokuwa Sovieti.

Wanawake hao wawili waliteuliwa na kundi la liberal Alde katika bunge la Ulaya.

Kiongozi wa kundi hilo Guy Verhofstadt amewataja kama "wanawake walio onyesha ujasiri mkubwa na ubinaadamu wakati wa uovu mkubwa".

Rais wa bunge la Ulaya Martin Schulz amesema ulikuwa "uamuzi wenye maana kubwa kuwasaidia waathiriwa hawa wawili waliokuja Uaya kama wakimbizi".

Maelfu ya watu wa kabila la Yazidi walilazimika kutoroka makaazi yao baada ya wapiganaji wa IS kuudhibiti mji uliopo kaskazini mwa Iraq, Sinjar mnamo Agosti 2014.