Twitter yatangaza kufunga huduma ya Vine

Vine Haki miliki ya picha TWITTER

Twitter imetangaza inasitisha huduma ya Vine inayowawezesha wateja kusambaza kanda za video wanazorikodi miaka minne baada ya kuzinduliwa.

Vine ilikuwa inawaruhusu watu kurekodi kanda fupi za video za sekundi sita zinazo jirudia zinapochezwa.

Twitter haikutoa sababu ya kufungwa kwa huduma hiyo lakini mapema Alhamisi ilitangaza inapunguza asilimia 9 ya wafanya kazi wake kufuatia ukuwaji mdogo wa mtandao huo wa kijamii.

"Katika miezi ya hivi karibuni , tutasitisha app ya [Vine]," Kampuni hiyo imesema katika blogu.

Twitter iliinunua huduma ya Vine kabla ya kuzinduliwa rasmi mnamo 2012, lakini imejumuisha video katika jukwa la Twitter, na pia kuzindua app ya kutazama video moja kwa moja kutoka kwenye mtandao Periscope.

Kampuni hiyo imesema app na mtandao huo hautofungwa moja kwa moja, na wateja watapewa fursa ya kuzidondoa na kuhifadhi video zao kutoka kwenye mtandao.