9 wauawa katika shambulio Maiduguri Nigeria

ramani

Watu 9 wameuawa na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa baada ya walipuaji wa kujitoa muhanga wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram kuushambulia mji wa Maiduguri uliopo kaskazini mashariki mwa Nigeria, maafisa wanasema.

Inaarifiwa kuwa washambuliaji hao walizunguka mjini ndani ya bajaji.

Mlipuko wa kwanza ulitokea wakati walipuaji wawili wa kujitoa muhanga walipojaribu kuingia katika kambi - ambayo maelfu ya watu wanaishi baada ya kulazimika kuyatoroka makaazi yao kufuatia kuzuka uasi.

Jamaa mmoja aliyeshuhudia mkasa huo ameeleza kuona watu waliojeruhiwa wakivuja damu.

Muda mfupi baadaye kumetokea mlipuko wa pili karibu na ghala la mafuta.

Jeshi la Nigeria limepiga hatua kubwa katika vita vyake dhidi ya Boko Haram.

Lakini wanamgambo hao wa kiislamu bado ni tishio na hutekeleza mashambulio ya kujitoa muhanga kila mara.