Mourinho ajipata taabani kwa mara nyengine

Mourinho baada ya kuondolewa katika eneo analokaa na kuelekezwa katika eneo la mashabiki
Image caption Mourinho baada ya kuondolewa katika eneo analokaa na kuelekezwa katika eneo la mashabiki

Mkufunzi wa Manchester United Jose Mourinho alifurushwa hadi eneo linalokaa mashabiki wikendi iliopita wakati wa kipindi cha mapumziko katika mechi ya matokeo ya sare ya bila kwa bila dhidi ya Burnley siku ya jumamosi.

Mourinho aliingia katika uwanja wakati wa kipindi cha pili cha mchezo na kuelekezwa katika kiti kimoja katika eneo la mashabiki katika uwanja wa Old Trafford huku timu yake ikipoteza pointi nane katika jedwali la ligi.

Baadaye kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 alielekea katika eneo la Wakurugenzi.

Refa Mark Clattenburg alikuwa amefutilia mbali aombi la Manchester United kwamba walifaa kupewa mkwaju wa adhabu baadaye katika kipindi cha pili.

Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya Mourinho kushtakiwa na shirikisho la soka nchini Uingereza FA kwa matamshi aliyotoa kuhusu refa Anthony Taylor mbali na kusema kuwa kuishi pweke mjini manchester ni mkasa.