China yaonesha hadharani ndege mpya za kivita

Two J-20 jets at Zhuhai airshow Haki miliki ya picha Reuters

China imeonyesha hadharani ndege zake mpya za kivita aina ya J-20 ambazo zina uwezo wa kujificha na kukosa kuonekana kwenye mitambo ya rada.

Ndege mbili za aina hiyo zilipaa angani kwa sekunde 60 wakati wa maonesho ya ndege ya Zhuhai katika mkoa wa Guangdong.

Maonesho hayo huwa makubwa zaidi nchini humo na huwakutanisha waundaji na wanunuzi wa ndege.

Ndege hizo zinatazamwa na wengi kama ishara ya hamu ya Beijing kuboresha na kuimarisha uwezo wake kijeshi.

Rais wa China Xi Jinping anataka kuimarisha majeshi ya nchi yake huku taifa hilo likiendelea kudhihirisha ubabe sana kuhusu umiliki wa maeneo ya bahari Kusini na Mashariki mwa China.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ndege ya kivita ya J-20 maonesho ya Zhuhai

Ndege hizo za J-20 zimeundwa na kampuni ya Chengdu Aircraft Industries Group, ambayo ni kampuni tanzu ya shirika la ndege la China ambalo kwa Kiingereza hufahamika kama Aviation Industry Corporation of China.

Baadhi wamelinganisha ndege hizo na ndege aina ya F-22 Raptor za Lockheed Martin.

Mchanganuzi wa masuala ya ndege Bradley Perret amesema ndege hiyo "bila shaka ni hatua kubwa katika uwezo wa kivita wa China".

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Ndege ya kusafirisha mizigo ya Y-20 pia imezinduliwa katika maonesho hayo ya Zhuhai

Ndege ya kwanza kabisa ya kubeba mizigo mizito ambayo imetengenezewa nchini China, ndege ya Y-20, pia imezinduliwa katika maonesho hayo.

Ndyingine zinazotarajiwa ni ndege kubwa ya AG-600 ya kusaidia katika uokoaji na kushika doria baharini.

Aidha, ndege ya kivita ya kuangusha mabomu kwa jina Xian H-6K na helikopta ya kutekeleza mashambulizi ya Changhe Z-10K zitazinduliwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii