Ajuza awafunza wanakijiji kujenga choo

Ana miaka 105 na wakakijiji wamefuata mfano wake kujenga choo
Image caption Bi Kunwar Bai Yadav alianza kampeini ya kujenga choo

Serikali ya India imeitangaza wilaya ya Dhamtari kama ya kwanza kufanikiwa kuwa na choo katika kila makaazi. Hii inamaanisha wakaazi wa eneo hilo lililoko katika jimbo la Chhattisgarh hawatumii vichaka au maeneo mengine yasiyo rasmi kwenda haja. Mafanikio haya yametokana na kampeini ya ajuza mmoja wa miaka 105 Bi Kunwar Bai Yadav.

Bibi huyu aliuza mifugo wake wachache na kujenga choo katika makaazi yake. Kitendo cha mama huyu kiliwavutia wanakijiji wenzake na eneo lote nzima ambapo watu walianza kujenya vyoo na kuacha kujisadia mahala popote. Bi Yadav amepata sifa kubwa siyo tu kwa wanakijiji bali na hata maafisa wa serikali ambayo inamtumia kama kielelezo za kampeini yao kuwashawishi watu kujenga vyoo.

Image caption Bi Yadav wa miaka 105 alikua wa kwanza kujenga choo kijijini mwake

katika miaka ya karibuni ajuza huyu anasema amekua akichoka sana kufanya safari kuelekea kichakani kwa haja. Anasema ameanguka mara kadhaa na kujeruhiwa wakati akienda kujisaidia huko kichakani.

" Nilianza kutafakari jinsi ya kujenga choo changu hapa nyumbani baada ya ushauri wa afisa wa mamlaka za jimbo. Hata hivyo sikua na fedha za kutosha. Niliamua kuchukua mali yangu pekee ya mbuzi 20 na kuwauza kwa dola 270. Mkaza mwanangu anayenitunza alichangisha fedha zaidi na tukafanikiwa kujenga choo chetu'', Amesema mama huyu.

Mapema mwaka huu Waziri Mkuu wa India Marendra Modi alitoa heshima zake kwa mama huyu kutokana na kampeini yake miongoni mwa jamii.Wilaya ya Dhamatari ina wakaazi laki nane na kila mmoja anatumia choo. Serikali ya India ilizindua kampeini ya kushawishi raia wake kutumia vyoo miaka miwili iliyopita.

Image caption Waziri Mkuu Narendra Modi ametoa heshima kwa Bi Yadav kutokana na kampeini yake

Hii ni baada ya takwimu kuonyesha kwamba raia milioni 550 wa India hawana vyoo na hujisaidia katika maeneo ya wazi. Kwa miaka mingi Bi Yadav alikwenda kichakani kujisaidia. Hata hivyo mwaka uliopita aliwauza mbuzi wake 20 na kujenga choo.

Baada ya kujenga choo chake, majirani wake walianza kumtembelea kuona chumba kipya na wao pia wakaanza kujenga vyoo kwenye makaazi yao. Katika mwaka mmoja wilaya nzima ilikua imejenga vyoo katika kila makaazi. Jimbo la Chhattisgarh limeanza kuandaa michezo ya kuigiza kuhamamisha jamii umuhimu wa kuwa na choo. Mfano bora ni wa mama Kunwar Bai Yadav.

Mkuu wa baraza la wanakijiji cha Barari anakoishi Bi Yadav amesifia bibi huyu na kusema " Awali watu hapa kijijini hawakupenda kujenga vyoo katika makaazi yao. Hii ni kwa sababu waliona ni sawa kujisaidia kichakani. Bibi Kunwar alitoa mfano kwao kwa kuanza kujenga choo na wengine wote wamefuata mfano huu. Kwa sasa kila nyumba ina choo chake."