Ripoti ya Zuma kuhusu ufisadi yatolewa

Maandamano yamekuwa yakifanyika kumtaka Zuma ajiuzulu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano yamekuwa yakifanyika kumtaka Zuma ajiuzulu

Idara ya kupambana na rushwa nchini Afrika Kusini imetoa ripoti iliyokuwa ikisubiriwa kuhusu uchunguzi kuwa familia tajiri ya Gupta ilikuwa na ushawishi mkubwa serikalini.

Ripoti hiyo inasema kuwa imetambua ushahidi unaoonyesha kuwa uhalifu huenda umefanyika katika viwango vya juu serikalini.

Imependekeza kuwa tume ya uchunguzi inayosimamiwa na hakimu ibuniwe ndani ya siku 30, kuchunguza madai ya ushawishi wa familia ya Gupta kwa uteuzi wa nyadhifa za serikali.

Tume hiyo mpya itawasilisha matokeo yake kwa rais ndani ya siku 180.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa bwana Zuma alikuwa amevunja sheria ya kuzuia ufisadi kwa kushindwa kuchunguza madai kuwa watu wawili walipewa nyadhifa za uwaziri na familia ya Gupta.

Haki miliki ya picha GALLO IMAGES
Image caption Mtoto wa Zuma (kulia) alikuwa mshirika wa kibiashara na familia ya Gupta

Awali Rais Zuma alisitisha jitihada zake kwa njia ya mahakama, kuzuia kutolewa kwa ripoti iliyotengenezwa na Madonsela.

Madonsela alifanya uchunguzi kuhusu madai kuwa Zuma aliruhusu familia tajiri ya Gupta kuwa na ushawishi mkubwa serikalini.

Makundi ya upinzani yamekuwa yakifanya maandamano kwenye miji mkubwa nchini Afrika kusini kupinga uongozi wa rais Jacob Zuma.