Kenya yatangaza kuondoa wanajeshi Sudan Kusini

Jemedari Johnson Mogoa Kimani Ondieki amefutwa kazi na UN Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jemedari Johnson Mogoa Kimani Ondieki amefutwa kazi na UN

Kenya imetangaza kuwa inawaondoa wanajeshi wake kutoka kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa cha kudumisha amani kilichoko Sudan Kusini, baada ya kamanda wake kutimuliwa kazini.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni imesema kuwa utaratibu wa kumuachisha kazi Jemedari Johnson Mogoa Kimani Ondieki haukuwa na uwazi.

Katibu Mkuu wa UN Ban Ki-moon alimfuta kazi Luteni Kanali Johnson Ondieki baada ya ripoti ya uchunguzi kusema alikosa kuwajibika kulinda raia mapigano yalipozuka upya nchini Sudan Kusini mwezi Julai.

Ripoti hiyo imesema walinda amani waliokuwa chini ya jemedari huyo hawakuchukua hatua yoyote wanajeshi wa serikali waliposhambulia kituo cha utoaji misaada mjini Juba na kuwadhulumu raia.

Kenya imesema uamuzi huo si wa haki na kutangaza kwamba itayaondoa mara moja majeshi yake yanayohudumu chini ya UN nchini Sudan.

Kadhalika, Kenya imejiondoa kutoka kwa mpango wa kutuma wanajeshi wa ziada kutoka nchi za kanda ambao walitarajiwa kutumwa kuimarisha kikosi cha UN nchini humo.

Kwenye taarifa yake, Kenya imesema kwa kumfuta Jenerali Gen Ondieki, Bw Ban alikosa kuangazia kiini cha matatizo yaliyobainika kwenye ripoti hiyo ya uchunguzi.

Kiir akubali wanajeshi zaidi wa UN Sudan Kusini

Wasanii Sudan kusini wachora kushinikiza amani

"Kilicho wazi ni kwamba Unmiss (Kikosi cha Walinda amani wa UN Sudan Kusini) inakabiliwa na matatizo ya kimuundo, ambayo yameathiri sana uwezo wake wa kutekeleza wajibu wake," taarifa hiyo imesema.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption UN ina wanajeshi 13,000 wa kulinda amani Sudan Kusini

Kenya inasema UN inafaa kuangazia matatizo ambayo yamekuwa yakikabili kikosi hicho badala ya kumlimbikizia lawama mtu mmoja.

Haijabainika Kenya ina wanajeshi wangapi Sudan Kusini kati ya wanajeshi 13,000 wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu Sudan Kusini.

Ubakaji

Watu kadha walikamatwa kuhusiana na matukio yaliyopelekea kufutwa kwa Jenerali Ondieki mjini Juba, maafisa wanasema.

Miongoni mwa waliokamatwa, wanane wanatuhumiwa kutekeleza ubakaji na wengine wanane uporaji.

Serikali ya Sudan Kusini ilikuwa inatekeleza uchunguzi wake kuhusu yaliyojiri Julai lakini ripoti ya uchunguzi huo haijafanywa wazi.

UN kufikia sasa haijajibu hatua ya Kenya ya kukataa uamuzi huo wa Bw Ban kumfuta kazi Jenerali Ondieki.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii