Ted Cruz: Nimempigia kura Trump

Bw Trump na Bw Cruz Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bw Trump na Bw Cruz walishambuliana vikali kampeni za mchujo

Aliyekuwa mpinzani mkuu wa mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump wakati wa mchujo wa kuteua mgombea wa chama hicho amesema amempigia kura Bw Trump.

Seneta wa Texas Ted Cruz, ambaye mara kwa mara alirushiana vijembe na Bw Trump, alitangaza hayo alipojiunga na mgombea mwenza wa Bw Trump Mike Pence eneo la Iowa kabla ya kuabiri ndege ya Trump-Pence kuelekea Michigan.

Baada ya kuulizwa maswali chungu nzima na wanahabari, Cruz alisema alimpigia kura Bw Trump Jumatatu.

"Ninafanya kila niwezalo tumshinde Hillary Clinton. Atakuwa mbaya sana iwapo atashinda urais."

Ameeleza kuwa suala muhimu litakuwa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Juu nchini Marekani.

Aidha, amesema ni muhimu sana kwa chama cha Republican kuendelea kuwa na wabunge wengi kwenye seneti.

Si zamani sana ambapo Cruz na Trump walikuwa wanarushiana matusi, wakiitana "panya", "muongo" na "mwoga".