Equatorial Guinea: Magari ya kifahari ya mwana wa rais yatwaliwa

Magari ya Teodorin Obiang Nguema Haki miliki ya picha AFP
Image caption Magari mawili kati ya yaliyotwaliwa

Waendesha mashtaka kutoka Uswizi ambao wamekuwa wakifanya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi wametwaa magari 11 ya kifahari yaliyomilikiwa na mwana wa kiongozi wa Equatorial Guinea.

Teodorin Obiang Nguema, mwana wa rais wa taifa hilo ambaye pia ni makamu wa rais, anatuhumiwa kulangua na kutakasa pesa.

Hajazungumzia tuhuma hizo kufikia sasa.

Maafisa wa Uswizi wametwaa jumla ya magari 11. Miongoni mwa magari hayo ni gari la Porsche la thamani ya zaidi ya $830,000 (£667,000) na Bugatti Veyron linalouzwa $2m (£1.7m).

Anatarajiwa kufika kortini Ufaransa kujibu mashtaka sawa na hayo mwaka ujao.

Waendesha mashtaka Geneva wanasema alinyakua utajiri wa mafuta wa taifa hilo na kuutumia kununua vitu vya anasa, vikiwemo ndege ya kibinafsi na kumbukumbu ya Michael Jackson.

Equatorial Guinea, taifa ndogo katika pwani ya Afrika, liligundua mafuta mwaka 1995.

Rais wake, Teodoro Obiang Nguema, ndiye aliyeongoza muda mrefu zaidi Afrika tangu atwae madaraka mwaka 1979.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Teodorin Obiang Nguema aliteuliwa makamu wa rais wa Equatorial Guinea na babake

Bw Obiang, 47, aliteuliwa kuwa makamu wa rais na babake mwezi Juni.

Anatarajiwa kufika Ufaransa kujibu mashtaka ya ufisadi na ubadhirifu wa pesa za umma. Amepinga madai hayo katika mahakama ya UN na kuna uwezekano kwamba hatafika mbele ya majaji Ufaransa.