Mwanamke mwenye 'macho ya kushangaza' afungwa jela Pakistan

Steve McCurry na picha za Sharbat Gula Hamburg, Ujerumani Juni 27, 2013. Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Sharbat Gula alipigwa picha na Steve McCurry (pichani), ambaye miaka 17 baadaye alimtafuta na kumpiga picha nyingine

Mwanamke kutoka Afghanistan aliyepata umaarufu duniani picha yake ilipochapishwa kwenye ukurasa wa kwanza wa jarida la National Geographic mwaka 1985 alipokuwa msichana amehukumiwa kufungwa jela.

Sharbat Gula amepatikana na hatia ya kuishi Pakistan akiwa na stakabadhi bandia za utambulisho.

Amehukumiwa kufungwa jela siku 15 na pia akatozwa faini ya takriban dola elfu moja za Kimarekani.

Atarejeshwa Afghanistan baada yake kutumikia kifungo chake.

Muda wake wa kutumikia adhabu umeanza kuhesabiwa tangu siku alipokamatwa. Hii ina maana kwamba kuna uwezekano wake kuachiliwa kufikia Jumatatu.

Sharbat Gula alitoroka Afghanistan ilipokuwa chini ya utawala wa muungano wa Usovieti.

Picha yake kama mkimbizi, ambapo alionekana kuwa na macho makali, iliibuka kuwa kama nembo ya madhara ya vita Afghanistan.

Macho yake yalikuwa na rangi ya kijani, jambo lililomfanya kufahamika kwa jina 'Green-eyed Girl'.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Sharbat Gula

Maafisa wanasema alikamatwa na Idara ya Uchunguzi ya Pakistan (FIA) baada ya uchunguzi wa miaka miwili Peshawar, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan.

Picha maarufu ya Bi Gula ilipigwa 1984 alipokuwa kambi ya wakimbizi kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Wakati huo wanajeshi wa Muungano wa Usovieti walikuwa wameingia Afghanistan.

Mwaka 2002, mpiga picha Steve McCurry alimtafuta na kumpiga picha. Wakati huo alikuwa anaishi kijiji kimoja Afghanistan akiwa na mumewe na binti zao watatu.

Baada ya kutokea kwa habari za kukamatwa kwa Bi Gula, Bw McCurry alisema atafanya kila juhudi kumsaidia kifedha na kisheria.