Ndege za Marekani zamuua kiongozi wa al-Qaeda

Farouq al-Qahtani, aliuawa na ndege za Marekani zisizokuwa na rubani Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Farouq al-Qahtani, aliuawa na ndege za Marekani zisizokuwa na rubani

Marekani imethibitisha kifo cha kiongozi wa cheo cha juu wa kundi la al-Qaeda, ambaye aliuawa na ndege za Marekani zisizokuwa na rubani Kaskazini Mashariki mwa Afghanistan mwezi uliopita.

Farouq al-Qahtani, kiongozi wa al-Qaeda eneo hilo aliuawa wiki mbili zilizopita.

Mzaliwa wa Saudi Arabia, al-Qahtani alikuwa kwenye orodha ya magaidi wanaotafutwa sana na Marekani mwezi Februari.

Alitajwa kuwa mmoja wa magaidi wanaopanga mashambulizi dhidi ya Marekani.

Msemaji wa serikali ya Afghanistan Abdul Ghani Mosamen, alisema wanamgambo 15 waliuawa wakati wa oparesheni hiyo iliyofanyika tarehe 23 mwezi uliopita katika mkoa wa Kunar.

Wale waliouawa ni pamoja na waarabu wawili na wapiganaji kadha wa Kundi la Taliban raia wa Pakistan.