Waandishi 9 wa habari wakamatwa Uturuki

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waandishi hao ndio watu wa hivi punde kukamatwa baada ya wanasiasa 9 kumatwa Ijumaa

Waandishi tisa wa habari kutoka gazeti la upinzani nchini Uturuki la Cumhuriyet, wamekamatwa na kuzuiliwa rumande kufuatia uamuzi wa mahakama mjini Istanbul.

Mhariri wa gazeti hilo, mchora vibonzo maarufu na mwandishi anayeikosoa serikali ni miongoni mwa wale waliokamatwa.

Waandishi hao ndio watu wa hivi punde kukamatwa baada ya wanasiasa 9 akiwemo kiongozi wa chama kinachowaunga mkono wakurdi cha HDP kukamatwa siku ya Ijumaa.

Gazeti la Cumhuriyet ni kati ya vyombo vichache vya habari vinavyomkosoa bwana Erdogan nchini Uturuki.

Waandishi wake wamehusishwa na kiongozi wa dini aliye nchini Marekani Fethullah Gulen, ambaye analaumiwa kwa kupanga mapinduzi ya mwezi Julai.