Clinton na Trump wajitayarisha kwa wikendi ya mwisho ya kampeni

Haki miliki ya picha AP
Image caption Donald Trump (kushoto), Hillary Clinton (kulia)

Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani, Hillary Clinton na Donald Trump wanajitayarisha kwa wikiendi ya mwisho ya kampeni.

Bwana Trump atazuru majimbo matatu muhimu yakiwemo Florida, Carolina Kaskazini, na Nevada, wakati Bibi Clinton akifanya kampeni Florida.

Kura za maoni za karibuni kabisa, zinaonyesha kuwa mgombea wa Democratic Hillary Clinton bado anaongoza, lakini yuko mbele kidogo tu ya mpinzani wake, Donald Trump.

Bwana Trump ametoa wito kwa wafuasi wake wasaidie kuzuia udanganyifu, na ameonya kuwa kunaweza kutokea ulalamishi kwenye uchaguzi.

Na huko Ohio, jaji wa serikali kuu, ameionya kampeni ya Bwana Trump, na ametoa amri kwa mshauri mmoja wa kampeni hiyo, aache kuwatisha wapigaji kura.