Mashabiki wa soka wauawa wakitazama mechi Sudan Kusini

Ramani inayoonyesha mji wa Juba

Watu 11 wameuawa na wengine 16 kujeruhiwa baada ya mtu mwenye bunduki kufyatulia risasi watu waliokuwa wakitazama mechi ya kandanda ya Ligi ya Premia katika mji ulio karibu na Juba, taarifa zinasema.

Gazeti la National Courier linasema mshambuliaji alifanikiwa kutoroka, licha ya maafisa wa usalama kufika eneo hilo "upesi".

Polisi wanachunguza kisa hicho, lakini kufikia sasa hawajabaini kilichochochea shambulio hilo.

Kisa hicho kilitokea katika mji wa Gure, katika viunga vya mji wa Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini.

Mji huo mkuu ulikumbwa na ghasia tena mwezi Julai baada ya wanajeshi waaminifu kwa Rais Salva Kiir na Dkt Riek Machar, aliyekuwa makamu wa rais, kukabiliana.

Dkt Machar alifutwa kazi na kuikimbia nchi hiyo.