Jeshi la Canada lachunguza kelele za ajabu kutoka bahari ya Arctic

Eneo la bahari ya Arctic Haki miliki ya picha GETTY IMAGES
Image caption Kelele hizo ziliripotiwa na watu wa eneo hilo kwamba zimewatisha wanyama na kuwafanya wakimbie mbali katika kipindi cha miezi michache iliyopita.

Jeshi la Canada limechunguza kelele za ajabu zenye mlio mkali zinazotoka kwenye sakafu ya bahari katika eneo lisiloweza kufikiwa kwa urahisi la kanda ya Arctic, maafisa wameiambia BBC

Kelele hizo za ajabu ziliripotiwa na watu wa eneo hilo kwamba zimewatisha wanyama na kuwafanya wakimbie mbali katika kipindi cha miezi michache iliyopita.

Ndege ya kijeshi imefanya msako wa aina mbali mbali wa kunasa sauti hizo, wamesema maafisa siku ya Ijumaa.

Hata hivyo jeshi hilo la Canada limesema hadi sasa haliwezi kuelezea sababu ya "sauti hizo za ajabu".

" Mhudumu wa ndege hiyo amesema hawakuweza kubaini kitu chochote cha ajabu kwenye uso wa bahari ama chini ya uso wa bahari ," imesema taarifa ya jeshi iliyotolewa kwa BBC.

" Kile ambacho alikiona ni makundi mawili ya nyangumi na sili wa bahari wenye pembe sita katika eneo lililochunguzwa''

Msemaji wizara ya usalama wa taifa mjini Ottawa amesema kuwa sababu ya kelele hizo - amazo wakazi wanasema zinaweza kusikika hata kupitia kuta za maboti zimesalia kuwa vigumu kutambuliwa.

Image caption Eneo ambalo llimekumbwa na kelele za ajabu

Sauti hizo ambazo zimekuwa zikisika katika kipindi chote cha majira ya joto katika maeneo ya baridi, mbunge Paul Quassa ameiambia CBC, yapata kilomita 120 kaskazini-magharibi mwa kijiji kidogo cha Igloolik.

Eneo hilo ni njia ya vijito vya maji katika Nunavut, eneo ambalo ni makazi mapya , makubwa na yenye kukaliwa na idadi ndogo ya watu nchini Canada, karibu na Greenland.

" Ni moja ya maeneo maarufu zaidi kwa shughuli za uwindaji nyakati za majira ya joto na baridi kwasababu ni eneo pana zaidi la maji lililozingirwa na barafu ambayo ina wanyama wengi wa baharini ," Amesema Bwana Quassa.

" Na wakati huu, majira haya ya joto, kulikuwa hakuna mnyama yoyote. Na hili likawa suala la kushangaza."

Maelezo mbali mbali kuhusu sauti hizo za kushangaza yamekuwa yakiwasilishwa katika vyombo vya habari nchini Canada.