Daniel Ortega na mkewe washinda uchaguzi Nicaragua

Rais Daniel Ortega na mkewe, Rosario Murillo Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Daniel Ortega na mkewe, Rosario Murillo, wakionyesha vidole gumba baada ya kupiga kura

Rais wa Nicaragua Daniel Ortega anatazamiwa kuongoza taifa hilo kwa muhula wa tatu mfululizo ibaada ya kujizolea zaidi ya 70% ya kura kulingana na matokeo ya awali katika uchaguzi wa Jumapili, wamesema maafisa.

Muasi huyo wa mrengo wa kushoto, Bw Ortega ni maarufu nchini humo kutokana na mipango yake ya kuimarisha maisha ya jamii na uchumi thabiti.

Alitarajiwa kwa kiasi kikubwa kushinda kwasababu hakukabiliana na upinzani yeyote.

Mkewe Ortega, Rosario Murillo, pia aligombea kama makamu wa rais.

"Idadi nzuri ya watu walijitokeza kupiga kura," alisema Telemaco Talavera, afisa anayehusika na uangalizi wa uchaguzi.

Huku 21.3% ya masanduku kutoka vituo vya kupiga kura yakiwa yamehesabiwa Bwana Ortega amepata 71.3% ya kura.

Wakosoaji wanamshutumu Bwana Ortega kwa kubadili mfumo wa kisiasa ili kuendelea kubakia mamlakani na kumaliza upinzani.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Ortega alikuwa ndiye mgombea aliyependwa sana raia wa Nicaragua

Ushindi wa Ortega haukuwa wa kushangaza- kulingana na Katy Watson, wa kitengo cha habari cha BBC cha Amerika ya kati.

Uchaguzi huo ulionekana kama wenye kuegamia upande mmoja nchini Nicaragua tangu kung'olewa madarakani kwa dikteta Anastasio Somoza mnamo 1979 - mchakato uliomuhusisha Bwana Ortega mwenyewe.

Lakini Nicaragua imegawanyika sana juu ya mpiganaji huyo wa zamani wa vita vya msituni mwenye umri wa miaka 70.

Wengi wanahisi kwamba uchaguzi huo uligubikwa na mizengwe, na suala hili kwamba , muhula huu ni wake wa tatu mfulurizo. Amekabiliwa na ukosoaji mkubwa nchini juu ya suala la mkewe kugombea kama mgombea mwenza na wengi wanasema ni suala sasa la kifamilia.

Ukweli unabakia kuwa pale pale, kwamba alikuwa ndiye mgombea aliyependwa sana.

Uongozi wake uliofanya uchumi wa Nicaragua kuwa thabiti katika ukuaji wake na ukosefu wa ghasia ikilinganishwa na matatizo yanayokumba majirani kama El Salvador na Honduras katika miaka ya hivi karibuni ni masuala yaliyompa sifa kama chaguo bora zaidi kwa wengi miongoni mwa raia wa Nicaragua.