Mtandao wa Ushahidi kuchunguza uchaguzi Marekani

Nembo ya mtandao wa Ushahidi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiga kura wataweza kuripoti matukio ya "vitisho dhidi ya wapiga kura, upotoshaji ama majaribio mengine ya kumzuwia mtu kupiga kura kupitia mtandao wa Ushahidi

Huduma maarufu ya mtandao wa uchunguzi wa mizozo uliyobuniwa nchini Kenya unaofahamika kama- Ushahidi, utatumiwa kuchunguza ghasia ama visa vya kukwamisha upigaji kura katika uchaguzi wa urais wenye ushindani mkubwa nchini Marekani, limeeleza gazeti la mtandao Quartz.

Mtandao huo ulitumiwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, na baadae ulirekodi matukio ya unyanyasaji wa kingono nchini Misri, na baadhi ya maeneo yanayohitaji msaada baada ya tetemeko la ardhi nchini Haiti 2012, mashambulio dhidi ya raia wa Syria, na uchaguzi wa 2015 nchini Venezuela.

Kuna hofu kwamba uchaguzi wa rais nchini Marekani unaweza kukumbwa na ghasia baada mgombea wa urais wa chama cha Republican Donald Trump kudai kwamba kutakuwa na wizi wa kura kwa ajili ya kumpatia ushindi wa mpinzani wake, Hillary Clinton.

Alisema pia kwamba atakubali matokeo iwapo tu atashinda na kuwataka wafuasi wake kuchunguza wale wanaopiga kura ili kuzuwia "ufisadi wa kura".

Hofu zake zilipuuziliwa mbali na maafisa wa uchaguzi.

Wapiga kura wataweza kuripoti matukio ya "vitisho dhidi ya wapiga kura, upotoshaji ama majaribio mengine ya kumzuwia mtu kupiga kura " kwa njia ya ujumbe,Twitter, au ujumbe kwa mtandao, kulingana na mtandao wa Ushahidi.