Uswisi kusaidia Tanzania kurudisha pesa zilizoibwa

Rais Magufuli amechukua msimamo mkali dhidi ya ufisadi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Magufuli amechukua msimamo mkali dhidi ya ufisadi

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Tanzania anasema kuwa nchi yake imetia sahihi makubaliano na Uswisi ya kusaidia kurudisha pesa ambazo zimefichwa kiharamu na raia wa Tanzania katika benki za Uswisi.

Augustine Mahiga alisema kuwa makubaliano hayo yana sehemu tofauti za ushirikiano zikiwemo za kubadilishana habari kuhusu uhalifu wa kiuchumi.

Wabunge wa upinzani nchini Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakiilaumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya maafisa na wafanyabiashara ambao wanakisiwa kuficha pesa zao nchi za kigeni.

Rais wa Tanzania John Magufuli amekuwa akipigana na ufisadi na matumizi mabaya ya pesa za umma tangu aingie madarakani mwaka uliopita.

Ripoti ya benki kuu ya Uswisi iliyotolewa mwezi Juni mwaka 2012 pmoja na matokeo ya uchunguzi wa chama cha wanahabari wa kimataifa iliiyochapishwa mwaka 2015, ilifichua raia wa wafisa nchini Tanzania wakiwemo matajiri wakubwa na maafisa wa ngazi za juu serikalini ambao walikuwa wameficha mamilioni ya dola katika benki za Uswisi.