Nani walimpigia kura Donald Trump?

Nani walimpigia kura Trump?

53%

ya wanaume - 41% walimpigia Clinton

42%

ya wanawake - 54% walimpigia Clinton

  • 58% ya Wazungu - 37% walimpigia Clinton

  • 8% ya Weusi - 88% walimpigia Clinton

  • 29% ya watu wa Hispania - 65% walimpigia Clinton

EPA

Donald Trump alimshinda Hillary Clinton uchaguzi wa urais nchini Marekani, jambo ambalo halikubashiriwa hasa kwa kufuata kura nyingi za maoni zilizokuwa zimefanya.

Wengi wamekuwa wakisema Bw Trump alipigiwa kura sana na wanaume Wazungu, wenye hasira, ambao wamechoshwa na jinsi Marekani inaongozwa.

Ili kupata utathmini kuhusu watu hasa waliompigia kura na kumsaidia kushinda, unaweza ukatathmini utafiti wa maoni wa baada ya kura kupigwa ambao ulifanywa na Edison Research kwa niaba ya kundi kwa jina National Election Pool, ambao ni mkusanyiko wa mashirika makubwa ya habari ABC News, Associated Press, CBS News, CNN, Fox News na NBC News.

Ni vigumu sana kupata sampuli ya kuwakilisha watu 120 milioni waliopiga kura. Ni utafiti mkubwa sana, ulioshirikisha wapiga kura zaidi ya 25,000, na hizi ndizo takwimu bora zaidi zinazoweza kupatikana kwa sasa. Hata hivyo, ni matokeo ya utafiti tu.

Kuna matokeo ya kushangaza, kwa mfano kwamba 10% ya watu wanaounga mkono mpango wa kujengwa kwa ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico walimpigia kura Bi Clinton.

Aidha, inashangaza kwamba 5% ya watu waliodhani rais ajaye anafaa kuendeleza sera za Barack Obama walimpigia kura Bw Trump.

Kumbuka kwamba jumla ya takwimu hizi huenda isitoshane na 100% kwa sababu si wote waliojibu maswali yote wakati wa kuhojiwa.

Kadhalika, kulikuwa na wagombea wengine wa urais waliopigiwa kura, na ambao walipata takriban 5% ya jumla ya kura zilizopigwa.

Matokeo hayo yanaonyesha 53% ya wanaume walimpigia kura Trump, na 41% wakampigia Bi Clinton. Takwimu hizo ni kinyume kabisa kwa wanawake, ambapo 53% walimpigia kura Bi Clinton na 41% Trump.

Miongoni mwa wapiga kura Wazungu (ambao ni 70% ya jumla ya wapiga kura), Bw Trump alishinda 58% naye Bi Clinton 37%, huku mgombea huyo wa Democratic akipata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wapiga kura Weusi - 88% na Bw Trump 8%.

Wapiga kura wa asili ya Hispania (Latino/Mexico), 65% kwa Clinton naye Bw Trump akipata 29%.

Ukiangalia sasa wanawake Wazungu, walimpendelea zaidi Bw Trump, ambapo 53% walimuunga mkono wakilinganishwa na 43% wakimpigia Clinton.

Imeripotiwa sana kwamba wapiga kura wa asili ya Hispania (Latino/Mexico) 29% waliompigia kura Bw Trump ni zaidi ya 27% waliompigia kura mgombea wa Republican Mitt Romney mwaka 2012, licha ya matamshi ya Bw Trump kuhusu Wamexico, kwamba ni wabakaji na walanguzi wa dawa za kulevya na kwamba atajenga ukuta mpaka wa Marekani na Mexico.

Bi Clinton alipata kura nyingi miongoni mwa watu wa mapato ya chini, wapiga kura 52% wanaopata chini ya $50,000 (£40,000) kila mwaka wakimuunga mkono, ikilinganishwa na 41% waliompigia kura mpinzani wake. Miongoni mwa wanaopata zaidi ya $50,000, walikuwa 49% waliompigia kura Trump wakilinganishwa na 47% kwaClinton.

Uungwaji mkono wa Clinton miongoni mwa wale wa kipato cha chini ya $30,000 ulikuwa chini ya aliopata Rais Obama mwaka 2012. Obama alipata 63% kutoka kwa kundi hilo ukilinganisha na 35% waliompigia kura Mitt Romney. Bi Clinton alipigiwa kura na 53% naye Trump 41%.

Kulikuwa pia na kubadili msimamo sana kwa wapiga kura wengi wasiosoma hadi kuwango cha diploma shule ya upili, Bw Trump akiongoza 51% dhidi ya Clinton 45%. Miaka minne iliyopita, Rais Obama aliungwa mkono na 64% wa kundi hilo akilinganishwa na Mitt Romney aliyepata 35%.

Bw Trump alishinda kura za watu wa mashambani 62% dhidi ya Clinton 34% na maeneo ya mitaa duni mjini 50% ukilinganisha na 45% za Clinton. Bi Clinton hata hivyo alishinda miongoni mwa watu wanaoishi mitaa rasmi, akipata 59% ya kura ukilinganisha na 35% za Trump.

Na Trump aliongoza pakubwa miongoni mwa watu wa umri mkubwa, miaka 45 kwenda juu. Clinton aliungwa mkono sana na wapiga kura wa umri mdogo.

Kulikuwa na taarifa, kabla ya uchaguzi, za wapiga kura wa Republican waliopanga kumpigia kura Bi Clinton kwa sababu hakumpenda mgombea wa chama hicho, Trump.

Lakini utafiti wa maoni ya baada ya upigaji kura unaonesha 7% kati ya wale waliojitambulisha kama wanachama wa Republican walimpigia Clinton. Hata hivyo, 9% ya waliojitambulisha kuwa wanachama wa Democratic walimpigia kura Trump.

Kati ya watu waliokubali kutoa maoni yao kuhusu mgombea waliyempigia kura, 41% kati yao walipenda sana mgombea huyo, 32% walikuwa na shaka kiasi na 25% walisema hawakupendezwa na wapinzani.

Kadhalika, miongoni mwa matokeo ya kushangaza ya utafiti huo, 18% ya waliohojiwa waliohisi kwamba Trump hakuwa amehitimu kuwa rais bado walimpigia kura, sawa na 20% waliohisi kwamba hakuwa na uvumilivu ufaao kiakili wa kuwa kiongozi.

Na 2% ya waliohojiwa walisema wataingiwa na wasiwasi iwapo Trump angeshinda lakini bado walimpigia kura, ikilinganishwa na 1% upande wa Bi Clinton ambao bado walimpigia kura licha ya kusema wangekuwa na wasiwasi iwapo Clinton angeshinda.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii