Maandamano nchi za Kiarabu yaligharimu $600bn - UN

Cairo, Misri Jumanne, Jan. 25, 201 Haki miliki ya picha AP
Image caption Maandamano yalikumba nchi za Kiarabu kuanzia 2011

Shirika la Umoja wa Mataifa limesema maandamano na maasi yaliyotokea nchi za Kiarabu kuanzia mwaka 2011 yamegharimu kanda hiyo karibu $614 bilioni.

Makadirio hayo ndiyo ya aina yake kufanywa na taasisi kubwa ya kiuchumi.

Hasara hiyo ni sawa na ukuaji wa uchumi wa 6% katika jumla ya mapato ghafi (GDP) katika mataifa ya kanda hiyo kati ya mwaka 2011 na 2015, Shirika la Uchumi na Masuala ya Kijamii ya Asia Magharibi (ESCWA) limesema.

Maandamano hayo na maasi, yaliyoanza Tunisia, yalisababisha kuondolewa madarakani kwa viongozi wa nchi nne na kuanzisha vita Libya, Syria na Yemen.

ESCWA ilitumia makadirio ya ukuaji wa uchumi ya kabla ya maandamano hayo ili kupata takwimu kamili ya hasara iliyopatikana.

Makadirio hayo yalijumuisha nchi ambazo hazikuathiriwa moja kwa moja na mizozo hiyo ya kisiasa lakini ziliathirika kwa njia nyingine, mfano kupitia kuwapokea wakimbizi, kupungua kwa fedha kutoka kwa raia walio nje ya nchi na kudorora kwa utalii.

Nchini Syria, ambapo maandamano dhidi ya serikali yalizaa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo sasa vinahusisha nchi za nje, hasara imefikia $259 bilioni.

Katika nchi ambazo zilifanikiwa kufanya mageuzi ya kisiasa, serikali mpya hazijatekeleza mageuzi ya kichumi yanayohitajika kutatua matatizo yaliyoanzisha maandamano hayo, ripoti ya ESCWA inasema.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii