Watakaoumia na watakaofaidi chini ya Trump Marekani

Rais mteule Donald Trump ataingia White House Januari 2017 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais mteule Donald Trump ataingia White House Januari 2017

Wamarekani wamemchagua mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump kama rais wao wa 45. Matokeo ya uchaguzi huo yaliwafurahisha wengi, lakini kwa wengi pia, masikitiko na huzuni.

Nani atafaidi na nani ataumia chini ya uongozi wa rais Trump?

Haya ni miongoni mwa tunayofahamu kutokana na hotuba alizotoa tajiri huyo hapo awali.

Pia maoni ya mgombea mwenza wa Trump, Mike Pence, gavana wa Indiana na Mkristo ambaye anatarajiwa kuwa kaimu rais yanafaa kuzingatiwa.


WANAWAKE

Jinsia ilichukua nafasi kubwa katika uchaguzi wa marekani ikilinganishwa na siku za hapo awali. Wapiga kura walikuwa na fursa ya kuamua kumchagua kwa mara ya kwanza 'rais mwanamke'.

Katika wiki za lala salama za kampeni, Mgombea wa Democratic Hillary Clinton alijaribu kuangazia shida ambazo Bw Trump amekuwa nazo kwa wanawake, kwa kumuita 'mnyanyasaji', mwenye historia ya miaka 30 ya historia ya, ''udhalilishaji, matusi na kuwashambulia "wanawake.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Hillary Clinton alisema Donald Trump ni mtu mfidhuli ambaye huwatusi na kuwadhalilisha wanawake, lakini wanawake wengi bado walimpigia kura

Lakini takwimu zinaonyesha wapiga kura wengi walitofautiana naye. Utafiti wa maoni wa baada ya upigaji kura unaonyesha asilimia 42 ya wanawake walimuunga mkono bwana Trump.

Asilimia 53 ya wanawake Wazungu walimpigia kura, huku asilimia 4 ya wanawake weusi wakimuunga mkono Trump, na mgombea mwenza wake Pence. Miongoni mwa wanawake Wakilatino, ambao bwana Trump bila shaka aliwatendea mengi maovu, asilimia 26 bado walimpigia kura.

Watarajie nini sasa?

Washindi

Kubaini kwa nini wanawake wangempigia kura bwana Trump, tovuti inayoegemea upande wa kushoto ilisema wanawake ambao wana nafasi ndogo za kujiendeleza katika sekta ya leba wangeunga mkono sera na maadili ambayo hutetea zaidi kugawanywa kwa majukumu na kazi nyumbani.

Wengi walivutiwa na ahadi za bwana Trump za kurejesha nafasi za kazi na ufanisi kwa wafanyikazi wa jamii ya wazungu na kuadhibu kampuni za marekani ambao zinatengenezea bidhaa zao nchi za nje.Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bintiye Trump, Ivanka, amesisitiza kwamba Trump ni mtu mzuri

Wanawake wajawazito na walioshiriki vita pia wamo katika nafasi nzuri ya kunufaika chini ya uongozi wa Trump. Mtoto wa Trump, Ivanka amemsaidia kubuni mpango wa malipo wa wiki sita kwa wanawake wanapopumzika kipindi cha kujifungua, kwa kampuni ambazo huwa haziwalipi marupurupu hayo.

Kwa wanawake walioshiriki vita, bwana Trump ameahidi kuwekeza katika matibabu ya "kuponya vidonda visivyoonekana" kama vile msongo wa mawazo kutokana na matukio ya kuogofya na mfadhaiko, na kuongeza idadi ya madaktari ambao wamehitimu kwa maswala ya afya ya kina mama.

Watakaoumia

Wanaharakati Wanawake wana wasiwasi jinsi Bw Trump atalichukulia suala la sheria ya utoaji mimba Marekani. Kwa hivi sasa, utoaji wa mimba unakubalika katika majimbo 50 kutokana na sheria ya Roe V Wade iliyopitishwa na mahakama ya juu mwaka 1973. Iwapo Trump atamteua mhafidhina kujaza nafasi iliyopo wazi kwa sasa katika mahakama hiyo, wahafidhina huenda wakabadilisha sheria hiyo.

Trump amelegeza msimamo wake kuhusiana na utoaji wa mimba kwa miaka mingi. Mwaka 1999 alisema: „Naamini katika uhuru wa watu kujiambulia. Lakini nachukia sana wazo la utoaji mimba. Nalichukia. Nachukia kila kitu kulihusu. Huwa napata kichefuchefu nikisikia watu wakilijadili. Lakini bado - bado naamini katika uhuru wa watu kujiamulia."

Mwezi Machi 2016, alifafanua : ''Msimamo wangu bado haujabadilika kama - Ronald Reagan, nasimamia maisha, lakina kwa masharti.''

Hisia ziliibuka aliposema kunafaa kuwa na adhabu ya aina fulani kwa wanawake wanaotoa mimba, iwapo jambo hilo lingeharamishwa - lakini baadaye akasema adhabu hiyo ingewalenga wale ambao wangetekeleza utoaji mimba.

Bw pence ameweka wazi kwamba anapinga kwa dhati utoaji mimba. Mwezi Julai, alisema: ''Mimi naunga mkono maisha, na siombi msamaha kwa hilo,". Aliongeza: Tutaiweka sheria ya Roe V Wade pahali inapostahili, kwenye rundo la majivu''.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mfuasi wa Hillary Clinton matokeo yalipoonyesha Trump alikuwa anaongoza

Waliomtuhumu Trump kwa kuwadhalilisha kingono pia wanastahili kuorodheshwa miongoni mwa watu walio sasa pabaya. Kampeini zake zilikubwa na madai kutoka kwa wanawake tofauti ambao aliwabusu au kuwapapasa bila idhini zao, na wengi wa Republican walihofia kuhusu uwezekano wake wa kushinda hasa pale video ya 2005 ilipofichuliwa na kumuonyesha akijitapa kwenye kipindi cha televisheni kilichokuwa kikiongozwa na mtangazaji Billy Bush, 'nilianza kuwabusu. Ni kama sumaku…ukiwa nyota hukuacha uwabusu na kuwapapasa."

Lakini ugombea wake uliponea kashfa hiyo na waliokuwa wanamlaumu sasa watausubiri kujua iwapo atatekeleza tishio lake kabla ya uchaguzi kwamba: "Waongo hawa wote nitawashtaki baada ya uchaguzi kumalizika."


WAISLAMU - WALIO MAREKANI NA NCHI ZA NJE

Katika taarifa iliyowapa wasiwasi Waislamu wa Marekani, Bw Trump hapo awali alikuwa ameitisha kuakikisha uchunguzi mkali unafanyika kwenye misikiti ya Marekani , akisema hajali iwapo ''si sawa kisiasa'' na kusema Waislamu wanafaa kufuatiliwa na vyombo vya dola kama njia ya kukabiliana na ugaidi.

Iliripitiwa kwamba Trump alitaka kuweka sajili ya Wamarekani wote Waislamu, lakini mwanachama huyo wa Republican baadaye alikanusha hilo na kusema mwanahabari alikuwa ameuliza hilo na kwamba hakulifahamu vyema swali hilo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Trump alishutumiwa kwa aliyoyasema kuhusu Khizr Khan, babake mwanajeshi wa Marekani Kapteni Humayun S. M. Khan, na mkewe Ghazala

Baada ya mwanahabari wa NBC kumuuliza swali Trump kuhusu tofauti kati ya kuwa na sajili ya Waislamu na sajili ya Wayahudi iliyowekwa na watawala wa Nazi nchini Ujerumani, Bw Trump alijibu: ''niambie wewe''.

Washindi

Ni vigumu kubaini faida dhahiri kwa jamii ya Waislamu kutokana na ushindi wa Trump.

Baadhi ya waandishi wa Kiislamu wameeleza wasiwasi wao kuhusu siku za usoni, wakisema ndilo kundi pekee la watu wachache ambao bwana Trump hajawarai kumuunga mkono kwenye kampeni.

Watakaoumia

Wakosoaji wamemlaumu mfanyabiashara huyo kwa kutumia chuki dhidi ya Waislamu na ubaguzi ili kuwarai wapiga kura ambao wanaogopa mashambulio ya kigaidi huenda yakatekelezwa nchini Marekani siku zijazo.

Bwana Trump aliwashambulia wazazi wa mwanajeshi wa marekani aliyeuwawa, Kapteni Humayun Khan, na hata kusema mamake Ghazala Khan ''hakuruhusiwa kuongea'' pamoja na bwanake katika mkutano mkuu wa chama cha Democratic National Convention kutokana na dini yake, jambo ambalo Bi Khan mwenyewe alilikana.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bw Trump wakati mmoja alipendekeza Waislamu wazuiwe kabisa kuingia Marekani

Baada ya ufyatuliaji wa risasi huko San Bernardino, California, ambapo watu 14 waliuawa, Bw Trump alitoa taarifa akitoa wito wa ''kufungiwa kabisa'' kwa Waislamu wasiingie Marekani ''hadi pale wabunge wan chi hiyo watakapobaini kinachoendelea.

Taarifa hiyo ililaaniwa kimataifa, na kuzua ombi la umma la kumpiga marufuku mfanyibiashara huyo kuingia Uingereza, ombi ambalo lilitiwa saini na maelfu ya watu.

Bw Pence mwenyewe alisema wito huo wa Bw Trump wa kuwapiga marufuku Waislamu ni wa kukera na kinyume cha katiba. Bw Pence wakati huo alimuidhinisha, Ted Cruz, mpinzani wa Trump katika uchaguzi wa mchujo jimbo la Indiana.

Inaonekana kama Bw Trump baadaye alibadili wazo hilo.

Hata hivyo, Mwezi Oktoba, Bw Pence aliulizwa na CNN kwa nini halizungumzii suala la kuwapiga marufuku Waislamu kutoingia Marekani. ''Naam, kwa sababu si msimamo wa Trump kwa sasa," alijibu.


WALATINO

Ukuta wa Mexico ni miongoni mwa ahadi alizozitoa wakati wa kampeini yake, ambazo zilizua utata zaidi. Aliahidi kuwarudisha makwao wahamiaji milioni 11 ambao hawana stakabadhi halali za uhamiaji.

Bw Trump alisema atakomesha wahamiaji haramu wanaovuka kutoka Mexico kuingia Marekani kwa ukuta huo wa mawe na saruji. ''Nitajenga ukuta mkubwa na hakuna anayeweza kujenga ukuta kama mimi, kwa bei ya chini," Bw Trump aliapa mwezi Juni mwaka wa 2015.

''Nitajenga ukuta mkubwa, ukuta mkuwa katika mpaka kusini mwa nchi yetu, na nitawafanya raia wa Mexico kuulipia ukuta huo.''

Washindi

Rais wa Mexico, Enrique Peña Nieto, amemtaja Bw Trump kama 'tishio' na amehakikisha hana nia ya kufadhili ujenzi wa ukuta huo utakaokuwa na urefu wa maili 2,000, unaotarajiwa kugharimu kati ya dola bilioni 8 na dola bilioni 25 za Kimarekani kulingana na makadirio ya jarida la Washington Post.

Lakini baadhi ya wakazi wa Kilatino mpakani wanaamini watanufaika iwapo mradi huo utatekelezwa, ujenzi huo utawanufaisha kupitia ajira.

Haki miliki ya picha Twitter / Donald Trump
Image caption Novemba 2015, Donald Trump alikariri wito wake wa kujenga ukuta mpaka wa Marekani an Mexico

Kwa asilimia 29 ya wapiga kura Wakilatino waliomuunga mkono bwana Trump, mambo mengi yalizingatiwa. Katika jarida la Washington Post, A.J. Delgado, Mlatino aliyemuunga mkono Trump alisema uhamiaji si jambo la kuzingatiwa kwanza, ''sisi tunajali kuhusu uchumi na kazi''.

Iwapo Trump ataweka ahadi yake ya kurejesha tena upatikanaji wa nafasi za ajira viwandani, walimuunga mkono watafurahia kumuunga mkono.

Watakaoumia

Wahamiaji 11 ambao wapo nchini Marekani kinyume cha sheria, ambao baadhi ni Walatino, wana kila sababu ya kuwa na wasiwasi. Bw Trump alisema angeongeza mara tatu, kikosi kilichopo cha kuwafurusha watu kutoka Marekani akiingia madarakani, na anaweza kuongeza idadi ya wanaotimuliwa hadi kufikia 1.2 milioni kwa mwaka.

Watalii wa kutoka Mexico, wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara hawatanufaika kwa ukuta huo, na karibu milioni moja huvuka mpaka huo kila siku. Wakosoaji wamesema biashara na Mexico imebuni nafasi za ajira zaidi ya ya milioni 6 nchini Marekani na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Watu karibu milioni moja huvuka mpaka kati ya Marekani na Mexico kila mwaka, wengi wao wakitafuta kazi

Mamilioni ya watu ambao hujumuisha jamii wa watu wa asili ya Kihispania wana misimamo tofauti ya kisiasa. Hawana msimamo mmoja kama wanavyodhani watu wengi, na ndiyo maana labda bado kunao waliopendezwa na sera za Bw Trump.

Kwa mfano, Miami, ni jimbo ambalo lina idadi kubwa ya raia wenye asili ya Cuba, msimamo mkali wa Trump kuhusu Cuba uliwavutia. Wamarekani waliotoka Cuba baada ya mapinduzi kwa muda mrefu wamekuwa wakipigia kura Republican kutokana na msimamo mkali wa chama hicho dhidi ya Wakomunisti.

Bi Clinton alipokuwa anatetea kuimarishwa zaidi kwa uhusiano kati ya Cuba na Marekani wakati wa kampeni, Bw Trump alitaka vikwazo vya kibiashara vibaki. Akiendelea kuwa na msimamo huo, maafisa wa Castro watakapozuru, wafanyabiashara ambao huenda wangefaidi kutokana na kuwepo kwa biashara huru wataumia.


Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii