Facebook yakana kumsaidia Donald Trump

Mark Zuckerberg akana facebook ilimsaidia Donald Trump kushinda uchaguzi
Image caption Mark Zuckerberg akana facebook ilimsaidia Donald Trump kushinda uchaguzi

Mwanzilishi wa mtandao wa facebook Mark Zuckerberg amesema kuwa atatumia kila njia kukabiliana na habari za uongo,huku akikana madai kwamba mtandao huo ulimsaidia rais mteule wa Marekani Donald Trump.

Katika chapisho lake katika mtandao wa facebook ,Zuckerberg amesema kuwa atatangaza mikakati ya kukabiliana na habari zisizo na ukweli hivi karibuni.

Amesema hatua hiyo itachukua muda mrefu ili kuhakikisha kuwa marekebisho yanayofanywa hayatakuwa na athari zozote ama upendeleo.

Ameongezea kuwa zaidi ya asilimia 99 ya habari zilizopo ndani ya mtandao huo ni za kweli.

''Ni habari chache sana zilizo na uwongo na utapeli.Utapeli unaoendelea haupendelei mtu mmoja wala hata siasa'', aliongezea.

Amesema kuwa haiwezekani kwamba utapeli uliopo ulibadilisha mwelekeo wa uchaguzi nchini Marekani.