Mvulana apigwa hadi kufa kwa kula mkate Kenya

Ramani ya Kenya
Image caption Ramani ya Kenya

Mtoto mmoja amefariki huku mwengine akiuguza majeraha baada ya kudaiwa kupigwa na shangazi yao kwa kula mkate katika kijiji cha Kiganjo kaunti ya Murang'a nchini Kenya.

Kulingana na runinga ya NTV nchini Kenya,Mtoto huyo wa miaka mitatu alifariki kutokana na majeraha aliyopata kwenye kichwa huku nduguye wa miaka 5 akiwa amelazwa katika hospitali ya Nyeri.

Wawili hao wanadaiwa kupigwa na shangazi huyo ambaye amedaiwa kuwa na akili punguani .

Majirani wanasema kuwa waliwasikia wavulana hao wakipiga kelele na kuelekea kuwaokoa kabla ya kuwapata wamelala ardhini wakiwa hawana fahamu.

Runinga hiyo inasema kuwa kulingana na mkaazi mmoja wa eneo hilo wavulana hao walikuwa wamewachwa nyumbani na bibi yao ili kukaa na shangazi yao.

Nilikuwa nimeenda kununua dawa ya mvulana mmoja kati yao baada ya ngozi yake kukumbwa na upele kabla ya kupata simu kutoka kwa mmoja wa jirani zangu akinielezea kilichotokea,alisema.

Kulingana na wakaazi wa eneo hilo Shangazi huyo aliwapiga wavulana hao baada ya kula mkate ambao ulikuwa wake.