Makamu wa rais asafiri na ndege ya kawaida Tanzania

Bi Samia Suluhu akiwa kwenye ndege Haki miliki ya picha Hisani
Image caption Bi Samia Suluhu akiwa kwenye ndege

Hamasa ya kutimiza lengo la kubana matumizi nchini Tanzania imeendelea kudhihirika sio tu kwa watendaji wa ofisi za umma bali pia katika ngazi za juu serikalini.

Takriban shilingi za Kitanzania zipatazo milioni 30 zimeokolewa na serikali baada ya makamu wa rais, Samia Suluhu kutumia ndege ya kampuni ya Tanzania, ATCL kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Safari hiyo imegharimu kiasi cha shilingi milioni saba badala ya takriban milioni 40 kama angetumia ndege ya kukodi kama ulivyo utaratibu wa kawaida kwa viongozi wa juu.

Bi Samia amesema pesa alizoziokoa zitakwenda kwenye matumizi mengine.

''nimeunga mkono agizo la Rais wetu, Dokta John Magufuli kuhusu kubana matumizi, kuonyesha uzalendo.Niliona mimi na msafara wangu tutumie ndege ya ATCL kwa gharama ya shilingi milioni 7.6 tu'', alisema.

Juma lililopita Ikulu ya Tanzania ilitoa picha ya Rais Magufuli akimjulia hali mkewe, mama Janeth Magufuli katika wodi ya Sewa Haji, hospitali ya yaifa, Muhimbili.

Haki miliki ya picha Hisani

Rais Magufuli amekuwa akilipa kipaumbele suala la kubana matumizi na kuelekeza pesa kutumika kwenye maeneo mengine kama vile katika sekta ya afya, elimu na kuboresha miundombinu

Miongoni mwa hatua alizochukua tangu kuingia madarakani ni kubadilishwa kwa utaratibu wa kusherehekea siku ya Uhuru mwaka huu, ambapo Magufuli alisema hatua hiyo iliokoa pesa nyingi ambazo hutumiwa katika maandalizi na kufanikisha sherehe hizo.

"Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe hiyo sasa zitumike kwa shughuli nyingine za kijamii ikiwa ni pamoja na kupambana na maradhi hasa kipindupindu, kununulia dawa za hospitali, vitanda vya hospitali na kadhalika kadiri kamati za maandalizi zitakavyoamua," alisema.