Mwanamgambo wa IS anayetafutwa na Italia akamatwa Sudan

Abu Nassim tayari anatafutwa nchini Tunisia kwa mashambulizi ya mwaka 2015 mjini Tunis Haki miliki ya picha AFP/GETTY
Image caption Abu Nassim tayari anatafutwa nchini Tunisia kwa mashambulizi ya mwaka 2015 mjini Tunis

Kamanda wa kundi la Islamic State, ambaye alihukumiwa bila ya kuwepo mahakamani nchini Italia kwa kuwaingiza watu kwenye ugaidi, amekamatwa nchini Sudan.

Abu Nassim ni raia wa Tunisia ambaye hadi siku za hivi karibuni, aliaminika kuliongoza kundi la wapiganaji wa Islamic State maeneo yanayozunguka bandari ya Sabratha nchini Libya.

Aliishi nchini Italia akiwa na umri wa miaka ya 20, ambapo alishukiwa kwa kujaribu kuwapa mafunzo ya itikadi kali wahamiaji wengine wa kiharabu, na kwa kupigana nchini Afghanistan na Syria kabla ya kuelekea nchini Libya mwaka 2014.

Abu Nassim alikamatwa na vikosi vya Marekani nchini Afghanistan mwaka 2001 na kusafirishwa hadi nchini Italia mwaka 2009, ambapo aliondolewa mashtaka yanayohusu ugaidi na kisha kusafirishwa kwenda nchini Tunisia mwaka 2012.

Alihukumiwa baada ya kukatwa rufaa Italia mwaka uliofuatia, lakini wakati huo tayari alikuwa nchini Syria.

Utawala nchini Tunisia ulitangaza waranti wa kukamatwa kwake, kafuatia mashambulizi kwenye makavazi ya Bardo mjini Tunis mwaka 2015, ambapo mtu mwenye silaha aliwaua watalii 21 na polisi moja.

Giacomo Stucchi, ambaye ni seneta anayeongozo kamati ya bunge ambayo inashughulikia masuala ya siri ya Italia, anasema kuwa majasusi wa Italia walichangia pakubwa katika kumuwinda Abu Nassim.