BBC World Service yatangaza upanuzi mkubwa zaidi 'tangu 1940'

BBC Broadcasting House
Image caption BBC World Service imeelezwa kuwa sehemu muhimu ya shirika la utangazaji la BBC

BBC World Service, kitengo cha shirika la BBC kinachohusika na utangazaji nje ya Uingereza, imetangaza kwamba itazindua idhaa 11 mpya katika upanuzi wake mkubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu "miaka ya 1940".

Upanuzi huo unatokana na ongezeko la ufadhili lililotangazwa na serikali ya Uingereza mwaka jana.

Idhaa hizo mpya zitatangaza kwa lugha za Afaan Oromo, Amharic, Gujarati, Igbo, Korea, Marathi, Pidgin, Punjabi, Telugu, Tigrinya, na Yoruba.

Idhaa hizo mpya zinatarajiwa kuzinduliwa mwaka 2017.

"Hii ni siku ya kihistoria kwa BBC, tunatangaza upanuzi mkubwa kabisa wa World Service tangu miaka ya 1940," amesema mkurugenzi mkuu wa BBC Tony Hall.

"BBC World Service ni kito cha thamani kubwa - kwa BBC na kwa Uingereza.

"Tunapokaribia kuadhimisha karne moja tangu kuanzishwa, ruwaza yangu ni ya BBC yenye kujiamini na kufikia watu wengi zaidi, jambo ambalo litafikisha uanahabari wetu bora ulio huru, usioegemea upande wowote pamoja na burudani kwa watu nusu bilioni kote duniani.

"Leo ni hatua muhimu katika kutimiza lengo hilo."

'Kuendelea kuwa muhimu'

Mpango huu unahusisha upanuzi wa idhaa katika nyanja ya dijitali ili kutoa huduma zaidi kwenye simu, makala za video na pia kuwepo zaidi katika mitandao ya kijamii.

IDHAA ZA BBC AFRIKA MASHARIKI

 • Swahili
 • Somali
 • Gahuza (Great Lakes - Kinyarwanda na Kirundi)
 • Oromo (kulenga Ethiopia na Eritrea)
 • Amharic (kulenga Ethiopia na Eritrea)
 • Tigrinya (kulenga Ethiopia na Eritrea)

Mnamo Jumatano, BBC itazindua huduma kamili ya dijitali kwa idhaa ya Thai, baada ya kufanikiwa kwa huduma ya Facebook pekee iliyozinduliwa mwaka 2014.

Mipango mingine ya upanuzi ni pamoja na:

 • kuongezwa kwa taarifa za habari za Kirusi, ambapo kutakuwa na makala tofauti kwa nchi jirani
 • kuimarishwa kwa huduma za televisheni barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuzinduliwa kwa vipindi 30 vipya vya runinga kwa ajili ya washirika Afrika kusini mwa jangwa la Sahara
 • vipindi vipya vya kuangazia kanda BBC Arabic
 • matangazo ya masafa mafupi na masafa ya wastani ya redio kwa wasikilizaji katika rasi ya Korea, pamoja na makala na habari za mtandaoni na mitandao ya kijamii
 • kuwekeza katika World Service English, kuhakikisha vipindi vipya, uanahabari wa kuaminika, na kupanua ajenda zinazoangaziwa kwenye taarifa

Fran Unsworth, mkurugenzi wa BBC World Service, alisema: "Nyakati za vita, mageuzi na mabadiliko ulimwenguni, watu kote duniani wametegemea World Service kwa habari huru, za kuaminika na zisizoegemea upande wowote.

"Kama shirika huru la utangazaji, tunasalia kuwa na umuhimu karne hii ya 21, wakati ambapo maeneo mengi duniani bado hayana uhuru wa kujieleza.

"Tangazo la leo linahusu kuiboresha World Service kwa kuwekeza katika siku za usoni

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mkurugenzi mkuu wa BBC Tony Hall anataka BBC iwafikie watu 500 milioni duniani kufikia wakati wa kuadhimisha karne moja tangu kuanzishwa, mwaka 2022

"Lazima tuwafuate wasikilizaji na watazamaji wetu ambao siku hizi wanapata taarifa kwa njia mbalimbali, kwa kuongeza idadi ya watu wanaofuatilia taarifa za World Service kupitia TV, na huduma nyingi sasa ambazo zimeingia katika dijitali.

"Tutaweza kuharakisha mageuzi katika mfumo wa dijitali, hasa kuwalenga vijana na watoto, na tutaendelea kuwekeza katika taarifa zaidi za habari kwa njia ya video.

"Kile ambacho hakitabadilika ni kujitolea kwetu katika kuendelea uandishi wa habari huru na usioegemea uapnde wowote."

Upanuzi huu utahakikidha kwamba BBC World Service sasa inapatikana katika lugha 40, ikiwemo Kiingereza.

Lord Hall ameiwekea BBC lengo la kufikia watu 500 milioni kote duniani kufikia wakati wa kuadhimisha karne moja tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022.