Aleppo yazidi kushambuliwa na watoto wauawa

Hospitali ya watoto ya Bayan baada ya kushambuliwa Haki miliki ya picha INDEPENDENT DOCTORS ASSOCIATION
Image caption Hospitali ya watoto ya Bayan baada ya kushambuliwa

Zaidi ya watu 30, wameuawa ikiwa ni siku pili ya mashambulizi ya anga katika maeneo yanayokaliwa na waasi mashariki mwa Aleppo nchini Syria.

Miongoni mwa waliouawa ni watoto na watoa misaada ya dharura, pamoja na kuharibu moja ya kituo kikuu cha afya ambacho ndio pekee kilibaki kuhudumia watoto, cha Bayan.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo anasema mashambulizi hayo yameharibu makazi katika sehemu ya chini ya jengo hilo karibu na maeneo walipo wagonjwa na madaktari.

Benki ya damu na gari la kubebea wagonjwa pia vinasemekana kuharibiwa na mabomu mazito.

Wanaharakati wanasema mashambulizi hayo ya anga yamewauwa watu 15, Mashariki mwa Aleppo na wengine 18 karibu na kijiji cha Batbo.

Mchambuzi wa BBC anasema kuwa mamia ya hospitali nchini Syria zimeshambuliwa na vikosi vya serikali na washirika wake tangu kuanza kwa mgogoro huo, kwa kile kinachoonekana kuwa ni mkakati maalum wa kuwalazimisha waasi kusalim amri.

Mada zinazohusiana