Trump ajitokeza kwa kushtukiza mgahawani New York

Donald Trump akiwa 21 Club mnamo 15 Novemba 2016 Haki miliki ya picha @RiggsReport
Image caption Trump alitembelea mmoja wa migahawa anayoipenda sana, mgahawa wa 21 Club

Rais mteule wa Marekani Donald Trump aliwashangaza wateja, na wanahabari wanaofuatilia safari zake, baada ya kujitokeza kwa kushtukiza katika mgahawa mmoja New York.

Wanahabari waliopewa kazi ya kufuatilia safari zake walibaki kushangaa kwani walikuwa wameelezwa kwamba angesalia nyumbani jioni hiyo.

Lakini badala yake, aliandamana na kundi ndogo la maafisa hadi kwenye mgawaha wa 21 Club katika mtaa wa Manhattan, mmoja wa migahawa anayoipenda sana.

Video zilizopigwa wakati wa kisa hicho Jumatano zinamuonyesha Bw Trump akiwasalimia wateja na kuwaambia kwamba atapunguza kodi wanayolipa kwa serikali.

Kuwasili kwake 21 Club kulijulikana baada ya mwandishi wa Bloomberg, Taylor Riggs, ambaye kibahati alikuwa ameenda kwenye mgahawa huo, alipakia kwenye Twitter ujumbe wa kusema kwamba Trump alikuwa amefika kwenye mgahawa huo. Hata hivyo, alikosea jina la eneo na badala yake akasema ilikuwa ni Keene.

Haki miliki ya picha @RiggsReport
Image caption Mwandishi huyo wa Bloomberg baadaye alijisahihisha kwamba ni 21 Club na wala si Keene

Kwneye video, Bw Trum anaonekana akiwaambia wateja: "Tutapunguza kodi mnayolipa, msiwe na wasiwasi kuhusu hilo."

Kundi la wanahabari waliopewa kazi ya kufuatilia safari za rais huyo mteule, inadaiwa waliambiwa na msemaji wa Bw Trump, Hope Hicks, mwendo wa saa 18:45 kwamba alikuwa amekamilisha shughuli za siku na kwamba walikuwa huru kwenda nyumbani.

Dakika 45 baadaye, msafara mkubwa wa magari ulionekana ukiondoka kutoka afisi kuu ya Bw Trump kwa sasa katika jumba la Trump Tower. Msafara huo ulijumuisha magari zaidi ya kumi na gari la kubeba wagonjwa.

Riggs alipoandika kwenye Twitter, wanahabari walikimbia mgahawa wa Keene kabla ya kugundua kwamba alikuwa 21 Club.

Hawakuruhusiwa kuingia Trump na familia yake walipokuwa wanakula chakula cha jioni kabla ya kiongozi huyo kuondoka na kurejea Trump Tower saa 21:41.

Hatua ya kutofuata desturi na kutowafahamisha wanahabari wanaomfuatilia rais mteule kuhusu safari hiyo imevitia hofu vyombo vya habari Marekani

Vyombo hivyo tayari vina wasiwasi kuhusu kunyimwa uhuru wa kufikia na kuzungumza na maafisa wa Bw Trump, na uwezekano wa kuzuiwa kupata habari zautawala wake kwa urahisi atakapoingia madarakani.

Bi Hicks baadaye aliwaambia wanahabari kwamba hakufahamu mipango ya Bw Trump na akaahidi kwamba wanahabari "watapata uhuru wa kufikia maafisa wa serikali na taarifa za serikali kama ilivyokuwa chini ya marais wengine".

Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya White House kimeshutumu kisa hicho. Viongozi wa chama hicho wamesema "haikubaliki kwa rais ajaye wa Marekani kusafiri bila waandishi wa habar wa kufuatilia habari zake na kuwafahamisha wananchi kuhusu alipo".

Rais wa chama hicho Jeff Mason hata hivyo amesema amepokea hakikisho kutoka kwa Bi Hicks lakini akasema wakati wa kutekeleza ahadi hiyo ni sasa na kusisitiza kwamba "waandishi wa habari wa kumfuatilia rais mteule wapo...kufuatilia shughuli zake anapoandaa serikali mpya".

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii