Mabaki ya meli yatoweka kwa njia ya kushangaza Indonesia

HNLMS De Ruyter Haki miliki ya picha Netherlands Institute of Military History
Image caption HNLMS De Ruyter iliyokuwa na mabaharia 345 ilikuwa chini ya Mholanzi Karel Doorman

Mabaki ya meli tatu za kivita za Uholanzi, ambazo zilikuwa zinahifadhiwa kama makaburi ya wakati wa vita, yametoweka kwa njia isiyoeleweka kutoka kwenye Bahari ya Java, wizara ya ulinzi ya Uholanzi imesema.

Meli zote tatu zilizamishwa na wanajeshi wa Japan wakati wa Vita vya Bahari ya Java mwaka 1942, wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Mabaki ya meli hiyo yaligunduliwa na wapiga mbizi mwaka 2002.

Ripoti katika gazeti la Guardian zinasema mabaki ya meli nyingine tatu za Uingereza yametoweka pia.

Serikali ya Uingereza imesema imesikitishwa sana na taarifa hizo na kwamba inafanya uchunguzi.

Wapiga mbizi waliotumwa mapema kwa maandalizi ya miaka 75 tangu kutokea kwa vita hivyo mwaka ujao walishangaa kupata mabaki ya meli hizo hayamo tena baharini.

Gazeti la Guardian linasema limeona picha za 3D, zinazoonyesha mashimbo makubwa kwenye sakafu ya bahari pahala ambapo mabaki ya meli hizo tatu - HMS Exeter, HMS Encounter na HMS Electra - yalikuwa, sawa na mabaki ya nyambizi ya Marekani.

Wataalamu wanasema ingechukua operesheni kubwa sana kuondoa mabaki hayo kutoka baharini.

Wizara ya ulinzi ya Uholanzi imesema inachunguza kutoweka kwa meli hizo.

Kupitia taarifa, wizara hiyo imesema mabaki ya meli mbili yote yametoweka, na sehemu ya meli ya tatu pia.

"Kuharibu makaburi ya vita ni kosa kubwa," wizara hiyo imesema.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imethibitisha kwamba imewasiliana na maafisa wa serikali ya Indonesia.

Msemaji wa wizara hiyo amesema: "Maisha ya watu wengi yalipotea katika vita hivyo na tunatarajia maeneo hayo yaheshimiwe na kutoguswa bila idhini ya Uingereza."

Theo Doorman, 82, mwanawe mkuu wa jeshi la wanamaji la Uholanzi Karel Doorman, aliyeongoza vita hivyo, alikuwa kwenye kundi la wapiga mbizi waliotaka kupiga picha mabaki ya meli hizo wiki mbili zilizopita.

Amesema hakuamini macho yake alipogundua mabaki ya meli hizo yalikuwa hayapo tena.

"Nilisikitika sana," alisema. "Sikukasirika. Hilo halikupeleki popote. Lakini nilihuzunika sana. Kwa karne nyingi ilikuwa desturi kwamba makaburi ya mabaharia huwa hayaguswi. Lakini hilo lilifanyika hapa."


Haki miliki ya picha Netherlands Institute of Military History

Vita vya Bahari ya Java

  • 27 Februari 1942
  • Wanajeshi wa Muungano walijaribu kuzuia wanajeshi wa majini wa Japan
  • Manowari za Uholanzi, Uingereza, Australia na Marekani zilishiriki
  • Meli kubwa tano na tisa ndogo za kutekeleza mashambulio, zikiongozwa na mkuu wa wanajeshi wa majini wa Uholanzi Karel Doorman
  • Ni meli mbili pekee zilizosalia
  • Meli zilizoangamizwa ni HNLMS De Ruyter, HNLMS Java, na HNLMS Kortenaer
  • Japana ilishinda vita hivyo na ikateka maeneo ya Dutch East Indies (sasa Indonesia)