Trump kukutana na waziri mkuu wa Japan

Shinzo Abe akihutubu mkoa wa Zhejiang, China 5 Septemba 2016.

Chanzo cha picha, Xinhua/AP

Maelezo ya picha,

Maelezo kuhusu mkutano huo hayajatolewa

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe atakuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya nje kukutana na Rais mteule Donald Trump, tangu kuchaguliwa kwake wiki iliyopita.

Shinzo Abe alisema anataka kujenga uaminifu na "kufanya kazi kwa ajili ya amani duniani", kabla ya kuondoka kuelekea Marekani kukutana na Bw Trump.

Mkutano huo ambao utafanyika mjini New York utafanyika huku kukiwa na wasiwasi kuhusu mwelekeo wa sera ya kigeni wa Marekani, ambayo ni mshirika mkubwa wa Japan.

Bw Trump kwenye kampeni alsiema Japan inahitaji kulipa zaidi ili wanajeshi wa Marekani waendelee kukaa katika ardhi yake.

Aidha, alishutumu mkataba mkubwa wa kibiashara ambao Rais Obama alitia saini na Japan na nchi nyingine za Pasifiki.

Marekani na Japan zimekuwa washirika wakubwa wa tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ambapo Marekani iliisaidia Japan kujenga upya uchumi wake.

Bw Abe atapitia New York akielekea Peru kuhudhuria mkutano wa nchi za Asia na Pasifiki.

Lakini maelezo kuhusu ajenda ya mkutano huo wa Alhamisi hayajatolewa. Aidha, haijaelezwa watakutana wapi hasa.

"Kumekuwa na utata mwingi," afisa wa Japan aliambia shirika la Reuters.

Japanese kuhusu ushindi wa Trump.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Bw Trump hakuonekana kupendwa sana na Japan wakati wa kampeni, ingawa kampeni yake ilivutia umma