Waathirika watoa ushuhuda hadharani, Tunisia

Sihem Ben Sedrine Haki miliki ya picha AFP
Image caption Sihem Ben Sedrine

Kwa mara ya kwanza Tunisia imesikiliza hadharani ushuhuda wa Waathirika waliotokana na matumizi mabaya ya madaraka, miongo kadhaa iliyopita.

Jumla ya watu sita wametoa ushuhuda wao, ikiwemo mama wa waandamanaji waliouawa mwaka 2011 na mke wa mwanaume aliyetoweka miaka ya 90 na baadaye kugundulika kuwa amekufa.

Televisheni ya Tunisia ilirusha moja kwa moja, ushuhuda huo uliokuwa ukitolewa chini ya Uratibu wa Tume inayohusika na masuala ya haki na utu inayoongozwa na Sihem Ben Sedrine na kuelezewa kama ni tukio la Kihistoria.

Kila muathirika wa vitendo hivyo alipewa takriban saa nzima kutoa simulizi zake ya yaliyomtokea kwa jopo la makamishna na washiriki wa mjadala huo wakiwemo Wawakilishi kutoka mashirika ya kiraia na Waangalizi wa kimataifa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waathirika wa matumizi mabaya ya madaraka Tunisia

Watu wa kwanza walioanza kutoa ushahidi walikuwa ni wanawake watatu ambao watoto wao wa kiume walipigwa risasi wakati wa ghasia za maandamano zilizotokea nchini humo miaka mitano iliyopita.

Ourida Kadoussi ni mmoja wao, anasema watoto wao waliuawa na hawakupewa haki zao.

Kwa upande wa tume hiyo, inaamini kuwa waathirika hao watawasamehe watu wanaowalalamikia, na kwamba walalamikiwa hao pia katika siku za karibuni watapata nafasi ya kutoa ushuhuda wao hadharani.

Hata hivyo waathirika hao wengi waliozungumza na BBC wametaka kulipwa fidia ya fedha na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

Zaidi ya matukio elfu 62, yakiwemo ya ubakaji na kuteswa yaliripotiwa katika tume hiyo tangu mwaka 2013.

Tunisia imekuwa nchi ya kidemokrasia baada ya kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Zine al-Abidine Ben Ali mwaka 2011.