IS yalipiza kisasi harusini Iraq

Iraq
Image caption Ramani ilikokuwa harusi

Majeshi ya serikali nchini Iraq wameeleza kuwa mtu aliyekuwa kwenye gari iliyosheheni mabomu alijitoa muhanga kwa kushambulia katika mkusanyiko wa watu waliokuwa wakisherehekea harusi na kuua watu kumi na saba na majeruhi kadhaa.

Shuhuda mmoja alielezea kuwa sherehe hizo zilikuwa zikiadhimishwa katika mji wa Ameriyat Falluja, upande wa Magharibi wa mji wa Baghdad, sherehe ambayo ilihudhuriwa na viongozi wa ngazi ya serikali ya maeneo hayo ambao ni wapinzani wakubwa wa kundi la wanamgambo wa dola ya kiislam, IS.

Kijana mmoja kutoka katika maeneo hayo eneo ambalo linahodhiwa na waumini wa madhehebu ya waislam wa Sunni, alijiunga na vikosi vya askari wa kikabila wenye lengo la kukabiliana na wanamgambo wa dola ya kiislam IS.

Kundi hilo la IS limekuwa katika hekaheka za kutimuliwa nchini Iraq hasa upande wa Kaskazini zaidi, ambapo nguvu kuu ya serikali ni kujaribu kuviondoa vikosi vya majeshi ya wanamgambo wa dola ya kiislam nje ya mji wa Mosul.