Urusi 'kuichokoza' Nato kabla Trump awe rais

Mchoro mkubwa wa Putin na Trump mjini Vilnius, Lithuania
Maelezo ya picha,

Mchoro mkubwa wa Putin na Trump mjini Vilnius, Lithuania

Lithuania imesema Rais wa Urusi Vladimir Putin huenda akaamua kuchokoza mataifa wanachama wa Nato kabla ya Donald Trump kuapishwa kuwa rais nchini Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Lithuania Linas Linkevicius amesema ana "wasiwasi mwingi" kuhusu nchi za Baltic, pamoja na jiji la Aleppo nchini Syria.

Shughuli ya mpito kabla ya kuingia madarakani kwa Donald Trump inafuatiliwa kwa karibu sana na mataifa ya Baltic.

Lithuania inaamini njama ya Urusi inaongozwa na sababu za kijiografia na kihistoria.

Lithuania ilikuwa sehemu ya Muungano wa Usovieti, lakini sasa ni mwanachama wa shirika la kujihami la nchi za magharibi Nato pamoja na Umoja wa Ulaya.

Inapakana na eneo linalomilikiwa na Urusi la Kaliningrad katika Bahari ya Baltic.

Katika mji mkuu, Vilnius, kuna mchoro mkubwa wa Trump na Putin wakiwa wamekumbatiana.

Serikali ya Lithuania kwa kawaida huwa haionyeshi wazi maoni yake lakini wakati huu imeeleza wazi msimamo wake kwamba urafiki kati ya Bw Trump na Bw Putin ni "hatari" kwa mataifa yanayoitegemea Marekani.

Maelezo ya picha,

Bw Linkevicius anahofia kuhusu mji wa Aleppo

Kuna wasiwasi kwamba Marekani inataka kuitazama Urusi kama mshirika na itakuwa vigumu kwa mataifa ya Ulaya Mashariki, ambayo yanatishiwa na Urusi, kujitetea.

Waziri wa mambo ya nje wa Lithuania Linas Linkevicius aliambia BBC: "Urusi si taifa kuu, ni tatizo kuu."

Urusi imesisitiza kwamba si tishio, na badala yake inailaumu Nato kwa kuzidisha uhasama kwa kupanua maeneo yake kwenda mashariki na kusafirisha silaha hadi maeneo yaliyo karibu na mpaka wa Urusi.

Bw Linkevicius amesema kuna hatari kwamba huenda Bw Putin akatazama kipindi cha sasa hadi wakati wa kuapishwa kwa Bw Trump Januari kama fursa ya kufanyia majaribio kujiandaa kwake kijeshi na pia nguvu za kidiplomasia za Nato.

"Utawala mpya utaingia madarakani nusu ya pili ya mwezi Januari," alisema.

"Nina wasiwasi sana kuhusu kipindi hiki, sio tu kwa sababu ya maeneo yaliyo karibu na Urusi bali pia kwa mji wa Aleppo, tutumai kwamba hawatakuwa wamepondwa kufikia wakati huo."

Lithuania inasema Moscow imekuwa ikiimarisha kambi yake kubwa ya kijeshi Kaliningrad.

Maelezo ya picha,

Meja wa jeshi la Lithuania Linas Idzelis amesema tishio kutoka kwa Urusi linaongezeka

Ni miaka 25 pekee tangu agizo lilipotolewa na Moscow kutuma vifaru kuwaponda waandamanaji waliokuwa wanapigania uhuru wa Lithuania mjini Vilnius.