UN: Idadi ya raia waliozingirwa na vikosi vya kijeshi Syria yaongezeka

O'Brien amesema mamia ya wananchi wa Syria wameuawa Mashariki mwa Aleppo wiki iliyopita
Image caption O'Brien amesema mamia ya wananchi wa Syria wameuawa Mashariki mwa Aleppo wiki iliyopita

Umoja wa mataifa umesema kuwa idadi ya raia wa Syria waliozingirwa na vikosi vya kijeshi imeongezeka na kufikia takribani milioni moja, ikiwa ni ongezeko la mara mbili zaidi katika kipindi cha miezi sita.

Raia hao wanaodaiwa kuzingirwa na vikosi vya serikali na kubakia katika maeneo yenye hatari, upweke, na ukosefu wa huduma muhimu za afya, pamoja na kulengwa na mashambulizi ya mabomu, kujeruhiwa na kuuawa lakini bado pia wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

Mkuu wa shirika la misaada la umoja wa mataifa Stephen O'Brien, amesema baraza la usalama la umoja huo lililazimika kuchukua hatua madhubuti ili kuwalinda raia wasilengwe na mashambulizi hayo.

Hata hivyo ameongeza kuwa hatua nyingine zilizochukuliwa na shirika hilo ni pamoja na kuanzisha utoaji misaada ya kibinadamu katika sehemu husika.

Image caption Siku ya Jumapili shule moja ililengwa na mabomu na kupelekea vifo vya wanafunzi nane

Awali washirika wa Syria, ambao ni Urusi, walizuia jitihada za utoaji misaada kwa raia katika maeneo hayo yaliyoathiriwa na vita.

Marekani imetaja majina kumi na matatu ya makamanda wa vikosi vya wapiganaji wanaodaiwa kuongoza, kuua na kujeruhi raia waliozingirwa katika katika eneo la mapigano.