Ndalichako: Wanaojiunga vyuo vikuu sharti wafaulu kidato cha sita

Tanzania Haki miliki ya picha Google
Image caption Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako

Kwa mara nyingine, Waziri wa Elimu nchini Tanzania Profesa Joyce Ndalichako, ametoa tamko linalozua mjadala mkali nchini humo.

Mara hii, ikiwa yaliyomo katika Hotuba yake yatatekelezwa, utakuwa mwisho wa moja ya mifumo iliyokuwepo ambapo mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne angeweza kuamua kusoma ngazi ya Diploma yaani Stashahada badala ya kupitia katika ngazi ya kidato cha sita.

Waziri huyo wa Elimu anaongeza kuwa wanafunzi wasiofaulu katika kidato cha nne wamekuwa wakienda kusoma ngazi ya cheti, kisha Stashahada na baadaye wakipenya na kuelekea katika Shahada yaani digrii lakini sasa watalazimika kupitia katika ngazi ya kidato cha sita.

Ambao hawatapitia katika safari ya kidato cha sita ni wale watakaofaulu katika kidato cha nne na kuchaguliwa kwenda kusoma katika vyuo vya ufundi daraja la kati.

Mfumo mwingine pia utakaaoathirika ni ule ambao mwanafunzi aliyehitimu kidato cha sita lakini akashindwa kukamilisha vigezo kadhaa vinavyotakiwa katika vyuo vikuu alikuwa anapata nafasi ya kufanya masomo ya muda yaani 'Foundation Course' katika Chuo kikuu huria cha Tanzania na kama angefaulu angeruhusiwa kuendelea na masomo ngazi ya degree.

Baadhi ya wale walioijadili hotuba hiyo hasa kupitia katika mitandao ya kijamii walionekana kumnukuu Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye hivi karibuni amesema njia bora ya kuboresha elimu nchini Tanzania ni wadau wa elimu kukutana katika meza ya mazungumzo ili wajadili changamoto zinazowakabili.

Waziri Ndalichako mara tu baada ya kuchukua madaraka aliondoa mfumo wa wastani wa pointi yaani GPA na kurudisha mfumo wa upangaji wa madaraja yaani division na katika kuhamasisha watu wafike ngazi ya chuo kikuu, katika siku za hivi karibuni Waziri huyo aliwatangazia wale wanaohitimu ngazi za chini za elimu kutovaa majoho na kofia kama wavaavyo wanaohitimu katika vyuo vikuu.