Kasisi awataka wanawake waache kupiga waume zao UG

Rais Museveni na mkewe walimkaribisha Papa Francis nyumbani kwao mwaka uliopita

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais Museveni na mkewe walimkaribisha Papa Francis nyumbani kwao mwaka uliopita

Kasisi mmoja wa kanisa katoliki mjini Kampala, Uganda, amewaonya wanawake akiwataka wakome kuwapiga waume zao, akisema kuwa wanastahili kuwaheshimu na kuwapenda, kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor.

Kasisi Cyprian Kizito alikuwa akilalamikia ripoti ya polisi katika wilaya ya Mpingi, iliyoonyesha kuwa kesi tano kati ya kumi zilizoripotiwa kuhusu dhuluma za nyumbani zilihusu wanawake wanaowapiga waume zao.

Gazeti hilo linamnukuu kasisi huyo wa Kampala akisema kuwa wanawake ni lazima wawakubali wanaume kuwa viongozi wa familia.

"Mnataka kuchukua madaraka kutoka kwa wanaume kwenye familia zenu? Nafikiri mnataka kumpinga Mungu ambaye hutuambia kuwa wanaume ndio viongozi wa familia," alisema Kasisi.

Pia katika gazeti ilo hilo , lakini kwa taarifa tofauti, chifu mkuu wa kabila la Acholi, Rwot David Onene Acana II amewaambia wanaume kuacha kuwahangaisha wanawake.

Hii inajiri huku rais Yoweri Museveni akianzisha kampeni ya kukabiliana na ghasia zinazoendeshwa kwa misingi ya kijinsia.