Mwanamfalme ataka wanawake waendeshae magari Saudi Arabia

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Prince Alwaleed amekuwa akikosoa kukandamizwa haki za wanawake nchi Saudi Arabia

Mwanamfalme mwenye ushawishi na mfanyibiashara tajiri nchini Saudi Arabia Alwaleed bin Talal, ameitaka nchi yake kuondoa marufuku inayowazuia wanawake wasiendeshe magari.

Saudi Arabia ndiyo nchi pekee duniani ambapo wanawake hawaruhusiwi kuendesha magari, na wanawake wanaharakati wamekamatwa kwa kukiuka marufuku hiyo.

Prince Alwaleed na mwanachama maarufu kutoka kwa familia ya kifalme ambaye amekosoa kukandamizwa haki za wanawake nchi Saudi Arabia siku za awali.

Amesema kuwa "kumzuia mwanamke asiendeshe gari leo hii, ni ukiukaji wa haki sawa na iliyomzuia mwanamke asipate elimu."

Taarifa ya Alwaleed iliyochapishwa kwenye mtandao wake inasema kuwa marufuku hiyo ni ghali mno nchini Saudi Arabia.

Zaidi ya madereva milioni moja huajiriwa kuendesha magari ya wanawake, wengi wakiwa ni raia wa kigeni.