Ndege iliyokuwa na timu ya Brazil iliishiwa na mafuta

Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Brazil ikipitia Bolivia Haki miliki ya picha AP
Image caption Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Brazil ikipitia Bolivia

Utawala nchini Colombia unasema kuwa kuna ushahidi kuwa ndege iliyokuwa imewabeba wachezaji ya klabu ya Brazil ilianguka baada ya kuishiwa mafuta ilipojaribu kutua.

Ndege hiyo haikuwa na mafuta ilipokuwa ikitua, afisa mmoja alisema, akinukuu sauti ya rubani aliyekuwa akiomba ruhusa ya kutua kutokana na kuishiwa mafuta na hitilafu ya mitambo ya umeme.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Visanduku vya mawasiliano ajali ya ndege ya Brazil

Mji wa Bogota ulitajwa wakati wa ratiba ya safari kama mahala ambapo ndege ingeongeza mafuta lakini ndege hiyo haikutua mjini humo.

Ndege giyo iliangua eneo lenye milima siku ya Jumatatu. Ni watu 6 kati ya 77 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walionusurika.

Ndege hiyo ilikuwa na timu ya Chapecoense ya Brazil ambayo ilitarajiwa kucheza fainali dhidi ya klabu ya Atletico Nacional mjini Medellin siku ya Jumatano.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mashabiki walikusanyika uwanja wa Atletico Nacional siku ambayo mechi hiyo ingechezwa

Timu hiyo ilisafiri kutoka mjini Sao Paulo hadi Santa Cruz ikitumia ndege ya kawaida ya abiria, kabla ya kubadilisha na kusafiri kwa ndege ya kukodishwa.

Rubani alikuwa na uamuzi wa kuongeza mafuta mjini Bogota, lakini akaamua kuelekea Medellin.

Alipokaribia Medellin, rubani aliomba ruhusa ya kutua kutokana na matatizo ya mafuta, lakini ndege nyingine kutoka shirika la ndege la VivaColombia ilikuwa ikisubiri kutua kutoka na kuvuja kwa mafuta.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mashabiki wa Chapecoense wakilia uwanjani

Rubani wa ndege iliyoanguka anasikika akiomba kwa dharura kuelekezwa kwa uwanja wa ndege kabla ya sauti hiyo kuzima.

Maafisa wanasema kuwa vifaa vya kurekodi sauti vitapelekwa nchini Uingereza kufunguliwa kwa uchunguzi.