Rais mteule wa Gambia kuwaachilia wafungwa wa kisiasa

Rais mteule wa Gambia Adam Barrow
Image caption Rais mteule wa Gambia Adam Barrow

Rais Mteule wa Gambia amekuwa akiongea juu ya anavyotazamia kubadilisha taifa tangu ashinde bila kutarajia juma lililopita.

Adama Barrow, ambaye alikuwa akifanya kazi kama mfanyabiashara wa kujenga nyumba na kuuza, alimshinda Yahya Jammeh, aliyenyakua madaraka kwa mtutu wa bunduki na kutawala kwa miaka 22.

Makundi ya haki za binadamu yamemlaumu Bw Jammeh kwa ukiukaji wa haki za watu wa mapenzi ya jinsia moja, waandishi wa habari na wanasiasa wa upinzani.

Rais Mteule wa Gambia amewahimiza watu waliotoroka Gambia kwa sababu ya hali ngumu ya maisha ya mtangulizi wake kurudi nyumbani ili kusaidia kujenga taifa lao.

Bwana Barrow aliambia shirika la habari la Associated Press kuwa atawaachilia kutoka gerezani wanasiasa wote wa upinzani walio gerezani.

Yeye pia alisisitiza kuwa atabadili msimamo wa awali wa Bw Jammeh wa kutaka kuondoa Gambia katika mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita, ICC, na Jumuiya ya Madola.

Raia wengi wa Gambia walikesha usiku wote wakisherehekea kuondoka kwa Bw Jammeh, ambaye amesema kuwa ataendelea na shughuli zake za kilimo.

Lakini changamoto nyingi zipo.

Taifa hilo ni maskini sana, na wananchi wengi wachanga wametorokea mataifa ya ng'ambo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii